Sunday, 22 October 2017

MCHAKATO WA UPIGAJI CHAPA MIFUGO NI HITAJI LA SERIKALI, SIYO HITAJI MUHIMU LA MFUGAJI.

 Na, Floidin John Linus
 
Kwanza, ieleweke sipo tofauti na agizo la serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kuhusu upigaji chapa wa mifugo ili kufanya utambuzi wa mifugo nchi nzima. Yawezekana serikali inakerwa na migogoro ya kila mara kati ya wafugaji na wa kulima. Matatizo ambayo yamekuwa yakiligharimu taifa na jamii kwa ujumla. Na hatimaye kuzorotesha kasi ya mpango wa serikali kuendeleza sekta ya ufugaji hapa nchini.

Lakini mtizamo wangu ni kuhusu chimbuko la huu mchakato wa upigaji chapa kwa kila halmashauri. Kwa miaka mingi sekta ya mifugo hapa nchini imeshikiliwa na wafugaji wadogo wadogo wanaofuga kwa mfumo wa asili na kizamani. Hali hii imechangiwa na ufugaji kwa kufuata mifumo ya asili na kitamaduni. Hata hivyo, mfumo wa kuhama hama kutoka eneo moja hadi lingine kulingana na upatikanaji wa malisho na maji ndio umekuwa chanzo cha migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Hebu tutizame mfano, migogoro inayoendelea kati ya wafugaji na maeneo ya hifadhi za mapori tengefu na hifadhi za wanyama pori. Sheria zinazosimamia maeneo haya ziko wazi sana kueleza adhabu anazopewa yeyote anayedhubutu kuvunja taratibu za uhifadhi wa maeneo yale. Hata wafugaji tunaofikiri wana tatizo la ukosefu wa elimu wanatambua vizuri sana lakini jambo la kujiuliza ni kwanini wanaweka pembeni adhabu kali na kuhatarisha mifugo yao kwa kuziingiza maeneo yale yanayolindwa kisheria???? 

Kila mara taarifa zinasambaa za upigaji minada mifugo iliyokamatwa ndani ya mapori tengefu lakini bado wafugaji wanadhubutu kuingiza mifugo ili kupata malisho. Je ni kweli tatizo ni elimu? kiburi? au tatizo ni nini?. Sasa kwa taswira hii ya mfugaji kudhubutu kuingia kwenye maeneo yanayolindwa kisheria anashindwaje kuingiza kwenye shamba la mahindi ambalo mmiliki wake yuko nyumbani. Sijaribu kutetea uharibifu huu lakini kuelezea jinsi serikali inavyotumia mbinu ya upigaji chapa kudhibiti migogoro na mfumo wa ufugaji wa kuhama hama.
Wakati mchakato huu unaanza wafugaji wengi  walipinga suala hili na serikali ikaona jambo la kufanya ni kuwaelimisha. Yawezekana kutoa elimu ikaonekana imechochea mwitikio lakini yawezekana pia wafugaji kuwa na uoga wa maagizo na sheria ndiyo chanzo cha mwitikio unaoendelea kujitokeza.
Lakini ukitumia jicho la tatu kutafakari maisha baada ya upigaji chapa bado changamoto zinazomkabili mfugaji zitakuwa hazijatafutiwa ufumbuzi. Bali itabaki uvunjifu wa sheria kwa kuingiza mifugo katika mikoa mingine kutafuta malisho na kuadhibiwa kisheria.Siyo rahisi mfugaji mkoani Dodoma wakati wa ukame atizame mifugo yake ikifa kwa njaa wakati mkoani Morogoro kuna malisho ya kutosha. Simaanishi kwamba naunga mkono ufugaji wa kuhama hama lakini serikali inatibu ugonjwa kwa dawa isiyokuwa sahihi. 
Serikali kupitia wizara ya mifugo na uvuvi iangalie namna ya kutatua mahitaji ya wafugaji ambayo yako wazi ili kuepusha huu ufugaji wa kuhama hama. Mfumo wa sheria pekee hautasaidia kutatua changamoto zinazomkabili mfugaji aliye nyikani. Changamoto zao ni zilezile miaka yote, wanahama hama kutafuta malisho,maji na miundombinu lakini upigaji wa chapa hautatui kero zao kuu zinazowakabili na kusababisha uzalishaji hafifu kulingana na kiasi pamoja na kiwango kinachotakiwa cha mifugo na mazao yake.

No comments:

Post a Comment