Malisho ndiyo muhimili mkuu wa
ufugaji sehemu yoyote hapa duniani. Ndiyo maana wafugaji wengi hapa nchini
wamekuwa wakizidi kusogea pembezoni mwa makazi ya watu ili kuwa na uhakika wa
chakula cha mifugo yao. Hata hivyo kutokana na sababu mbalimbali zinazokumba
wafugaji wamelazimika kuhama hama kutoka eneo moja hadi jingine ili kutafuta
malisho haswa wakati wa kiangazi. Mfumo huu wa kuhama hama hata hivyo haujawa
suluhisho la malisho kwa wafugaji bali umezidi kusababisha matatizo mbali mbali
kama kueneza magonjwa na migogoro. Hata, wengine wakaenda mbali wakaelezea
mfumo wa kuhama hama unavyochangia uharibifu wa mazingira, japokuwa si
wana-ikolojia wote wanaokubaliana na dhana ya mfumo wa kuhama hama kama una
madhara kwa mazingira (nami ni mmoja wapo) na kila kundi lina sababu zake za
kisayansi zenye kuthibitishika. Lakini lengo letu si kupambanisha hizi dhana
mbili tofauti. Lengo langu ni kueleza kwanini mfugaji atazidi kuteseka na
malisho kama hakutakuwa na mpango mkakati wa kupambana na hali ya malisho hapa
nchini. Sababu chache kati ya nyingi zilizopo ni kama zifuatazo;
1.
Mabadiliko
ya tabia ya nchi yatazidi kuwa endelevu hivyo kusababisha ukosefu wa mvua ya
kutosha ama kutokunyesha kwa muda muafaka. Kama hakuna unyevunyevu wa kutosha
kwenye udongo tunategemea kukosa uzalishaji mzuri wa nyasi za kutosha ndani ya
machunga hali itakayomlazimu mfugaji kuhama eneo.
2. Ongezeko
la idadi ya watu linaendana na uhitaji wa ardhi kwa ajili ya makazi, miundo
mbinu, huduma za kijamii n.k. Hivyo tutegemeee ardhi kuzidi kuhitajika zaidi.
Kadri siku zinavyoenda tunaona ukuaji wa idadi ya watu mijini na vijijini,
maeneo mengi ya malisho yamevamiwa na watu kwa ajili ya makazi na kupunguza
machunga sana.
3. Mabadiliko
ya kiuchumi yanaambatana na ongezeko la mitaji, hivyo uwekezaji kwenye ardhi
utazidi kuongezeka. Kwa ajili ya kilimo, viwanda n.k. Hali hii imezidi
kujitokeza katika mikoa mbalimbali hapa nchini. Ni kwa ajili ya maendeleo ya
nchi lakini mfugaji anaathirika kwa namna moja ama nyingine.
4. Maeneo
wanayochungia wafugaji si maeneo wanayoyamiliki kisheria ni ama ya vijiji au
maeneo ya wazi ya serikali. Hivyo yanapotokea mabadiliko ya matumizi ya ardhi
tutegemee ukosefu wa malisho. Maana yangu ni kwamba wanakochungia ni maeneo
yaliyotengwa na serikali za vijiji au maeneo ya wazi. Maeneo haya
hayatuhakikishii uwepo wa malisho ya uhakika kwa sababu ya ukosefu wa uangalizi
wa kitaalamu na mabadiliko ya matumizi ya ardhi.
5. Ukosefu
wa mikakati ya kusimamia, kuboresha na kutunza maeneo ya machunga. Hali hii
imesababisha kuwe na ongezeko la mimea vamizi na kuharibu malisho kwa kiasi
kikubwa. Katika maeneo ambayo wafugaji wanalishia yamekuwa yakizidiwa kwa wingi
wa mifugo (carrying capacity) na kusababisha upotevu wa ubora wa udongo, mmomonyoko
wa ardhi, uharibifu wa malisho, uvamizi wa vichaka n.k. Lakini japo na
changamoto hizi kwenye malisho ya pamoja kumekuwa hakuna usimamizi wa kutosha
ili kulinda afya ya machunga.
6. Wafugaji
kutokuwa tayari kubadili mfumo wa zamani wa ufugaji ili kuendana na mabadiliko
ya sasa. Huu si muda wa kuhama hama na mifugo kama awali. Dunia imebadilika
wafugaji wanatakiwa kupata akili ya kijasiriamali, ufugaji iwe fursa ya
kibiashara. Wawe tayari kubadilisha mfumo wa ufugaji, aina ya mifugo, kulima
malisho na uvunaji wa mifugo kwa wakati. Hii itasaidia kuendana na mabadiliko
ya ulimwengu wa sasa.
7. Tatizo
la ki-sera hapa nchini kuhusu malisho, mbegu za malisho na wataalamu wa kutosha
wa usimamizi wa nyanda za malisho.
Upatikanaji wa mbegu bora za malisho zenye kuendana na mazingira ya nchi
yetu.
Ø
Katika hayo yote ukosefu wa wataalamu wa kutosha
wa malisho kunasababisha elimu hii iwe finyu sana kwenye jamii. Hata hivyo hili
ni suala liko katika uwezo wa serikali yenyewe.
Suluhisho la changamoto ni kubadili
mfumo mzima wa ufugaji na kufuga zaidi kisasa kwa kuangalia mazingira na masoko
ya mifugo na mazao yake. Makala kuhusu malisho yatazidi kutolewa tuwasiliane
zaidi kwa ushauri wa malisho.
No comments:
Post a Comment