Monday, 9 October 2017

HEI (HAY) BORA NI IPI?

Na, Floidin John Linus,     Email. floidinjohn@gmail.com
Wafugaji wengi hapa nchini wamekuwa wakikosa uhakika wa chakula cha mifugo kwa
Nyasi zikifungwa kuhifadhiwa
msimu(mwaka) mzima wa uzalishaji. Hii ni kutokana na kutegemea zaidi vyanzo asilia vyenye kuwezesha uwepo wa malisho na maji. Hata hivyo kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi, ongezeko kubwa la uhitaji wa mazao ya mifugo na ongezeko la watu, mfumo wa uzalishaji hauna budi kubadilika zaidi na kuwa wa kisasa. Kuweza kuendana na mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo kwa kiasi kikubwa yanaathiri ufugaji kutokana na upungufu wa malisho msimu wa ukame.
Kama nilivyowahi kuandika namna bora ya kuandaa shamba la nyasi HAPA ili kuweza kupata uhakika wa chakula cha mifugo. Hata hivyo baada ya kuvuna kama ilivyoelezwa katika LINK hapo ya kustawisha shamba la nyasi, mfugaji au mkulima anaweza kuhifadhi nyasi katika mfumo wa nyasi kavu au hei (hay). 
Kuvuna nyasi na kuzihifadhi kwa mfumo wa nyasi kavu ni bora zaidi kwa sababu huzuia upotevu wa chakula kwa kukanyagwa na kuchafuliwa hovyo na wanyama, badala yake mfugaji huweza kulisha kulingana na mahitaji.Hata hivyo kwa vile, hei ndio mfumo unaotumika zaidi kuhifadhi nyasi kwa ajili ya mifugo, mfugaji lazima atambue sababu zinazosababisha ubora wa hei pamoja na namna ya kutambua hali ya ubora wa hei aliyoitunza.
Hei iliyofungwa vizuri
Ubora wa hei haswa hutizamwa kwa kiwango cha virutubisho(nutrients) kilicho ndani ya nyasi hizo. Kiwango cha protini, nyuzi nyuzi (fiber content) na umengenywaji(digestibility) huweza kutumika kutambua ubora wa hei iliyohifadhiwa.
Hata hivyo kwa mfugaji wa kawaida hawezi kupata uwezo wa kufanya tafiti maabara kutambua ubora wa nyasi alizohifadhi. Hivyo anaweza kulinganisha ubora wa chakula(hei) kwa kuangalia kiwango cha uzalishaji cha mnyama anachotakiwa kuwa nacho, mfano kiasi cha maziwa na ongezeko la uzito. Ijapokuwa uzalishaji hafifu siyo tu sababu ya ukosefu wa lishe duni, kuna sababu nyingine pia kama hali ya hewa na magonjwa, hivyo majawabu ya maabara ni bora zaidi.
 Jambo la kuzingatia ni kwamba, hapo juu nimeongelea zaidi kutambua ubora wa hei kwa kuangalia hali ya mnyama zaidi. 
Tunapozungumzia ubora wa hei, unaweza ukasababishwa na vyanzo mbali mbali na kusababisha kuongezeka au kushuka kwa ubora wa hei inayozalishwa na mfugaji kwa ajili ya mifugo au biashara.
Shamba la nyasi
Sababu hizo ni kama vile,
  • Aina ya nyasi, nyasi hutofautiana kiwango cha virutubisho na madini kwa ajili ya mifugo. Pia vile vile uwezo wa kufyonza katika udongo na ukuaji wake.
  • Ukuaji wake, ubora wa hei hupotea haraka kadri nyasi zinavyozidi kukomaa. Hivyo mfugaji  hushauriwa kuvuna nyasi mapema kabisa baada ya kuanza kutoa maua.
  • Hali ya hewa na utunzaji wake,  mfano baada ya kuvuna mvua ikinyeshea nyasi husababisha upotevu wa virutubisho. Pia vilevile jua kali husababisha upotevu wa Vitamini A na kupukutika (kuvunjika vunjika) kwa majani.
  • Kiasi cha mbolea kwenye udongo, kiwango cha kutosha cha madini ya chokaa, nitrojeni, fosifeti (phosphate), Potassium (K) na madini mengine yanayohitajika kwa kiasi kidogo ni muhimu kwa ajili ya kuzalisha hei yenye ubora.
KILIMO CHA NYASI NI BIASHARA INAYOLIPA.

No comments:

Post a Comment