Na, FLOIDIN JOHN LINUS floidinjohn@gmail.com
Ni ukweli usiopingika kwamba wafugaji wengi wa kitanzania ni wale wenye
shughuli hii kama asili yao mfano wasukuma na wamasai. Jamii hizi ndizo
zimekuwa chanzo kikubwa cha mifugo na mazao ya mifugo katika masoko na
minada yetu hapa nchini na nje ya nchi.
Lakini kama ufugaji ndio utamaduni wao je, ni kweli tuna sababu ya
kupoteza utamaduni wao?
Jibu ni hapana,bali kusaidia kuboresha mfumo wa ufugaji kuhakikisha kuwa
mfugaji anafaidika na ufugaji wake wa kila siku kwa ajili ya kuongeza
kipato na kustawisha uchumi wa nchi.
Mambo makuu mawili kwa mfugaji wa kitanzania yanayomkuba ni mabadiliko
ya tabia nchi pamoja na ongezko kubwa la watu ambalo linazidi kuimega
ardhi ya malisho kwa shughuli mbalimbali kama makazi na kilimo.
Kuendana na hali hii ya mabadiliko kuna kila sababu ya mfugaji kuona
sasa umuhimu wa kujikita katika kilimo cha malisho ya mifugo. Hii ina
maana kwamba mfugaji atatakiwa kununua ardhi na kujikita katika kilimo
cha malisho ili kuhakikisha ustawi wa mifugo yake kwa mwaka mzima.
Kilimo hiki kinahitaji ushauri wa kitaalamu haswa kuweza kutambua aina
ya majani yanayoweza kustahimili kulingana na eneo analopatikana
mfugaji. Ni kweli kuna gharama zake lakini faida yake ni kubwa zaidi
kuliko kutangatanga na mifugo katika kipindi ambacho malisho
hayapatikanai. .Kilimo cha malisho kinampa mfugaji uwezo wa kuvuna nyasi
hadi mara nne kwa mwaka na kujitengenezea uwezo mkubwa wa kuhudumia
mifugo yake. Aidha, kilimo cha malisho kitapunguza kutembeza mifugo
umbali mrefu zaidi kwa ajili ya kutafuta malisho jambo ambalo huharibu
ubora wa nyama, hudhoofisha mifugo na kuipunguzia uwezo wa kuzaliana
(reproductive efficiency).
Katika msimu wa mvua malisho huwa ni mengi sana, uwezo wa ardhi
kuzalisha malisho huongezeka na hivyo mifugo hupata chakula kiurahisi,
lakini huu ndio msimu ambao wafugaji wetu wanatakiwa kujifunza namna ya
kuhifadhi chakula kwa ajili ya baaadae. Mfano kuacha baadhi ya maeneo
bila kuyachunga hadi msimu wa kiangazi ndio yachungiwe ili kuilinda
mifugo hadi msimu mwingine.
.
Mfugaji anaweza kuvuna pia nyasi na kuziandaa kwa ajili ya hei(HAY)
baadae kuzifunga vizuri na kuzitunza hadi msimu wa kiangazi ambapo
hakuna malisho kwa wingi. Kama mfugaji atakuwa na uwezo wa kuvuna mara
nne kwa mwaka, manake atakuwa na uwezo wa kuzalisha hay nyingi zaidi ili
kuilinda mifugo yake msimu wa kiangazi isihangaike na chakula.
.
Njia nyingine ni katika mfumo wa saileji(silage), inahitaji utaalamu
zaidi lakini mfugaji akiweza kuelekezwa tu basi anaweza kuhifadhi
chakula cha mifugo kwa mfumo huu pasipo kupoteza ubora wa chakula hicho.
Huku ndiko tunakotamani tuwaone wafugaji wakiamkia huku na kunufaika na
ufugaji. Mifugo ni utajiri lakini uelewa huu ni tafsiri iliyo mbali na
wafugaji wetu. Dhana ya wingi wa idadi ya mifugo ndiyo dhamira ya
wafugaji. Lakini kama wakiruhusu utaalamu uingilie katikati yao watavuna
zaidi kwa idadi ndogo tu ya mifugo.
Tunayo safari ndefu ya kufika tunakotamani cha msingi ni kutonyosheana
mikono na kutafutiana chuki bali kuamka na kumsaidia mfugaji atoke huko
aliko na twende naye karne ya 21 tunakokutizama katika mfumo wa
kibiashara
No comments:
Post a Comment