Mfumo wa kuvunia maji yanayotiririka. |
Uvunaji wa maji (rain water harvesting) ni teknolojia inayotumika
kukusanyia na kutunzia maji kwa ajili ya shughuli mbalimbali. Hata
hivyo kuna njia nyingi au aina tofauti za uvunaji wa maji.
Hata hivyo makala ya leo ni kutoa mtizamo wangu kwa wafugaji wa
kitanzania(pastoralists) wanaoishi ama kufanya shughuli za ufugaji
katika mikoa yenye changamoto ya ukame, mfano Dodoma, Manyara, Singida,
Shinyanga na baadhi ya maeneo ya Morogoro.
Wafugaji wa kitanzania wamekuwa wakiathiriwa sana na tatizo la
uchelewaji wa mvua za vuli. Husababisha ukosefu wa malisho na maji kwa
ajili ya mifugo na wafugaji wenyewe. Aidha, kutotabirika kwa mvua pamoja
na kiwango kidogo cha mvua ni changamoto katika shughuli ya ufugaji
hapa nchini.
Katika msimu wa ukame wafugaji wamekuwa wakihama kutoka sehemu moja hadi
nyingine kuhakikisha kwamba wanapata mahitaji ya mifugo yao kama vile
malisho na maji. Hata kama sehemu wanazoishi zina nyasi bado hulazimika
kusafiri umbali mrefu kutafuta maji kwa ajili ya mifugo. Kuhama hama
kumekuwa kukisababisha hasara nyingi sana kama vile, migogoro ya mara
kwa mara, uharibifu wa vyanzo vya maji, kupoteza muda mwingi ambao nguvu
kazi ingetumika kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo, kukosesha
haki watoto ambao wana umri wa kwenda shule, uzalishaji hafifu wa mifugo
sababu mifugo hutumia nishati kubwa sana kusafiri umbali mrefu hivo
kupunguza ufanisi wa kushika mimba, ukuaji na uzalishaji wa maziwa na
nyama iliyo bora zaidi.
Hata, hivyo wafugaji wetu wanaweza kutumia teknolojia mbadala ya kuvuna
maji wakati wa masika na kuyatunza hadi msimu wa ukame kipindi ambacho
kuna changamoto ya maji. Kiasi kikubwa cha maji wakati wa msimu wa mvua
hutiririka juu ya uso wa dunia (surface run-off) na kusababisha matatizo
makubwa kama mafuriko, mmonyoko wa ardhi na uharibifu wa miundombinu.
Eneo lililoathirika na mafuriko |
Matatizo haya yamekuwa yakitokana na uwanda mkubwa unaokuwa tambarare na
wenye ukosefu wa uoto wa kutosha kuzuia madhara ya maji yanayotiririka
kwa kasi. Hata hivyo hatuwezi kupuuzia changamoto ya ubovu wa miundo
mbinu katika kuchangia tatizo la mafuriko haya.
Wafugaji wana uwezo mkubwa sana wa kutumia fursa ya mvua inayonyesha
ndani ya muda mfupi kwa mwaka katika maeneo yao kwa ajili ya kupambana
na chanagamoto zinazosababishwa na ukame kwa upande wa ufugaji. Ni
dhahiri kabisa, suala la mabadiliko ya tabia ya nchi linaathiri kila
sekta hapa nchini. Hivyo basi, hata serikali tunayoitegemea ina kazi
kubwa kupambana na mabadiliko haya kwa sekta zote. Lakini suala la
uvunaji wa maji bado wafugaji wanaweza kulifanya kwa ufanisi mkubwa
pasipo kuhitaji msaada wa kifedha kutoka serikalini labda tu ushauri wa
kitaalamu pekee. Wafugaji wana hazina kubwa, mifugo ni hazina iliyobeba
utajiri wa wafugaji. Wanatakiwa kujifunza kutokana na hasara kubwa
wanayopata kila mara tunapokumbana na hali ya ukame hapa nchini. Kuna
njia rahisi za kuvuna maji bila kutumia vifaa na zana za gharama kubwa
kuandaa eneo la kuvunia maji. Kwa hazina ya mifugo waliyonayo wafugaji
si jambo kubwa wala gumu kutumia hata teknolojia za asili (local
technology) kuandaa eneo la kuvunia maji yatirirkayo msimu wa mvua.
Teknolojia ya asili ya kuvunia maji |
Huweza kufanywa kwa kufata mkodo au mteremko wa uelekeo wa maji lakini pia kama eneo linabeba kiasi kikubwa cha maji njia ya kuhamisha(divert) baadhi ya kiasi cha maji kuelekea eneo la kuvunia huweza kutumika pia.
Teknolojia ya asili ya kuvunia maji |
FAIDA ZA KUVUNA MAJI.
Faida za kuvuna maji ni nyingi sana,lakini ntajaribu kuorodhesha baadhi tu,
- Kunyweshea mifugo msimu ambao maji hayapatikani ndani ya eneo husika kutoka kwenye vyanzo vingine.
- Matumizi ya nyumbani kwa ajili ya familia.
- Kumwagilizia malisho kama mfugaji ataamua kuzalisha malisho kwa ajili ya mifugo yake, hivyo kuhakikisha uwepo wa chakula cha mifugo.
- Kupunguza tatizo la mmomonyoko wa ardhi.
- Kupunguza tatizo la mafuriko kama kiasi kikubwa cha maji kitavunwa ili maji yasipotee bure.
- Kuboresha hali ya ufugaji, sababu mifugo haitosafiri umbali mrefu kutafuta maji hivyo nguvu kubwa ya mnyama itaelekezwa kwenye ukuaji na uzalishaji.
- Kupunguza tatizo la migogoro na watumiaji wengine wa ardhi.
No comments:
Post a Comment