Unapohitaji kujikita
katika ufugaji kwa mlengo wa kibiashara yaani kuzalisha mifugo au bidhaa za
mifugo kitu muhimu cha kujiuliza ni chakula cha mifugo.
Mfugaji anaweza fikiria
chakula katika mfumo wa nyasi kavu (hay) au nyasi mbichi. Hata hivyo wafugaji
wengine wanaweza kufikiri mbali na kuamua kulima nyasi zao binafsi kwa ajili ya
mifugo au/na kuuza.
Tofauti na wengi wanavyofikiri, mahitaji ya mbolea katika
uzalishaji wa nyasi ni makubwa kama katika uzalishaji wa mazao ya kawaida.
Udongo wenye rutuba ya kutosha na matumizi sahihi ya mbolea huweza kutoa kiasi
kingi cha malisho ya mifugo.
Mfugaji kabla ya kulima
shamba kwa ajili ya malisho anashauriwa kutafuta wataalamu wa malisho ili
kuweza kumsaidia kufanya utafiti katika eneo husika. Hata hivyo kwa kujikita
katika rutuba ya udongo na uzalishaji, aina tofauti za nyasi huitaji mazingira
tofauti ya kiwango cha madini ndani ya udongo. Si vyema mkulima kuamua kulima
nyasi bila kupata ushauri wa kitaalamu.
Katika kilimo cha nyasi changamoto ya
rutuba kwenye udongo kwa kiasi kikubwa ni Nitrojeni (N), ikifuatiwa na
Fosiforasi(P), Potashiamu (K) na salfa(S) kwa nadra sana katika udongo wa
kichanga.
Katika udongo wenye rutuba nzuri
ukiambatana na kilimo cha umwagiliaji wa nyasi au mvua ya kutosha tunategemea
kupata malisho mengi zaidi kwa sababu nyasi zitapata rutuba na maji ya kutosha. Hata hivyo, maeneo yenye kutegemea mvua tu kama ardhi ina rutuba ya kutosha
bado uzalishaji wa nyasi unakuwa ni mzuri.
Virutubisho vyote ambavyo
mwanadamu anategemea kutoka kwenye nyama vinatokana na virutubisho ambavyo
vinachangiwa na malisho anayokula mnyama pia. Lazima mfugaji apate malisho bora
ili kuzalisha mifugo na mazao yake yenye ubora wa juu pia.
Mfugaji unaweza kuona kwa namna
gani rutuba ya udongo ni muhimu katika ufugaji. Katika nchi yetu si rahisi
kupata wafugaji wataoweza kufanya kilimo cha malisho cha umwagiliaji bali wengi
wanategemea mvua za msimu hivyo lazima kujikita katika ubora wa udongo na elimu
ya utunzaji wa udongo ili kutoruhusu upotevu wa rutuba.
Kwa hakika mfugaji
akiweza kudhibiti upotevu wa ubora na rutuba ya udongo tunategemea kupata
matokeo chanya kwa kutegemea tu mvua ya msimu. Ni rahisi kugundua upungufu wa
madini katika udongo kwa kuangalia viashiria kadha wa kadha katika uoto wa juu
ya ardhi lakini hii inahitaji utaalamu na uzoefu pia.
Hata hivyo, siyo kila uzalishaji hafifu katika malisho husababishwa na upungufu wa rutuba pekee katika udongo. Mkulima/mfugaji anatakiwa kupata ushauri wa kitaalamu kabla ya kuamua kutumia mbolea katika uboreshaji wa kilimo cha malisho.
No comments:
Post a Comment