Wednesday, 8 November 2017

CHLORIS GAYANA (RHODES GRASS)

Na Floidin John 
floidinjohn@gmail.com
Hii ni aina ya nyasi inayostawi katika udongo wa aina tofauti kichanga, tifutifu, mfinyanzi n.k. Lakini katika udongo wenye asili ya asidi na maeneo yenye kivuli ustawi wake ni hafifu sana. 

Inastawi katika eneo lolote lenye kupokea wastani wa mvua kuanzia 500mm-1200mm lakini pia katika maeneo yenye kupata wastani wa mvua hadi 1800mm aina hii ya nyasi imedhibitika kustawi vizuri pia. Jotoridi la ustawi wa Rhodes grass ni 25 ̊C hadi 35˚ C.

 Kwa mfugaji mwenye uwezo wa kulima na kutumia njia ya umwagiliziaji ni faida zaidi kwani huongeza uzalishaji wa malisho. Huweza kupandwa kwa kutumia vioteo (vegetatively propagated) au mbegu (seeds).

Ni nyasi nzuri kwa wafugaji kutokana na uwezo wake wa kuzalisha malisho  msimu wa kiangazi pia. Ina uwezo wa kustahimili kiangazi kwa takribani miezi 6. Uwezo huu unatokana na uwepo wa mizizi mirefu yenye urefu wa hadi takribani mita 4.25 ardhini ambayo huwezesha kupata maji ya kutosha kwa muda mrefu.  Uwezo wake wa kustahimili moto na mazingira yenye ardhi yenye madini ya chumvi chumvi ni faida pia kwa wafugaji wenye ardhi ya aina hii.

JINSI YA KUANDAA SHAMBA


  • Fatilia taarifa sahihi kutoka mamlaka ya hali ya hewa ili kutambua mvua za masika zinatazamiwa kuanza wakati gani
  • Andaa shamba kwa kutumia trekta (ploughing and harrowing) na kupata udongo laini uliopondwa vizuri (fine seedbed)
  • Changanya mbegu (seeds) na mchanga, udongo wa kawaida au unga wa mbao.
  • Mwaga (broadcast) kwenye shamba zima kwa njia kama ya kupanda mchicha au mtama. Lakini mkulima anatakiwa kupita shambani baada ya kuchipua ili kuangalia kama hakuna sehemu iliyowazi bila mbegu kuota ili kurudishia. Kama unatumia vioteo angalau acha nafasi ya sentimeta 40 kati ya shimo na shimo na kati ya mstari na mstari.
  • Kama ardhi inahitaji mbolea,hii itategemea na ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu wa malisho
  • Mkulima anaweza kuchanganya nyasi hizi na mikunde kama,  Clitoria ternatea, Stylosanthes spp, Macroptilium atropurpureum, Medicago sativa na Centrocema pubescens. Hii itasaidia kuongeza malisho, chanzo cha protini na Nitrojeni kwa Rhodes grass.
  • Udhibiti wa magugu vamizi hufanyika taratibu kwa mikono au kemikali kutokana na uwezo wa nyasi hizi kudhibiti uvamizi wa magugu.
Kama hali ya hewa ni nzuri udongo unapata unyevu nyevu wa kutosha, mkulima anaweza kuvuna
nyasi kwa takribani misimu mitatu kwa mwaka. Hivyo basi, hatushauri mfugaji kuchungia kwenye shamba lake la kuzalisha nyasi ili kuweza kuweka usimamizi mzuri.

Mfugaji anashauriwa kuvuna nyasi mara baada ya kuona zinaanza kutoa maua(flowering stage) au kabla ya hapo kidogo. Muda huu ni mzuri zaidi kuandaa hei (hay) yenye ubora zaidi lakini kuchelewa kuvuna nyasi kutasababisha kuvuna nyasi zilizokomaa sana ambazo hazifai kwa kifugo.
Mbegu zinapatikana ni wakati muafaka wa wafugaji wetu kujikita katika kilimo cha malisho sasa.

No comments:

Post a Comment