Monday, 9 October 2017

UMUHIMU WA MTI WA MLUSINA KATIKA UFUGAJI.

Leucaena leucocephala
Kwa jina la kisayansi unaitwa Leucaena leucocephala.
Kwa kiingereza huitwa Leucaena au Lead tree.
Kiswahili huitwa mti wa Mlusina.

Mmea huu jamii ya mikunde(leguminous) asili yake ni Mexico. Lakini hapa nchini pia hustawi vizuri kabisa. Ni kati ya miti yenye jamii ya mikunde inayokua kwa haraka sana. Ni chanzo cha chakula kwa mifugo . Hupandwa pembeni ya shamba kama kuonesha mpaka wa shamba, kutoa kivuli, kizuia upepo(wind breaker), kuzuia mmomonyoko wa ardhi au maalumu kwa ajili ya chakula cha mifugo. Mti huu ukiachwa kwa takriban mwaka 1.5 huruhusu mzizi mkuu kuingia ndani zaidi ya udongo hivyo  kuhakikisha uzalishaji wa chakulacha mifugo hata wakati wa kiangazi kipindi ambacho hakuna chakula cha kutosha au ubora wa malisho unapokuwa mbovu.
Shina laini na majani yake ni chanzo kizuri cha protini kwa mifugo na virutubisho vingine kama carotenoids na  vitaminslakini pia huambatana na asidi-amino iitwayo mimosine ambayo huwa  na athari endapo chakula kinachotokana na jamii hii ya mikunde kitatumiwa pasipo uangalifu, haswa wanyama wenye tumbo moja(monogastric) kama nguruwe, kuku na sungura huathirika zaidi na huweza kusababisha kifo kwa wanyama hawa.
Mlusina hufananishwa na mkunde mwingine (alfaalfa) muhimu kwa wingi wa virutubisho haswa protini kwa ajili ya mifugo. Lakini  Mlusina una upungufu wa sodium na iodine lakini una wingi wa b -carotene.

                                         MAANDALIZI YA MLUSINA KWA AJILI YA MIFUGO
Majani ya mlusina yaliyoandaliwa kama chakula cha mifugo
Maandalizi ya mlusina kwa ajili ya chakula cha mifugo huandaliwa kwa kuondoa majani pekee kutoka kwenye matawi ya mlusina. Ni kwa sababu ndiyo sehemu ya mmea huu yenye kuwa rahisi zaidi kutumiwa na mifugo(digestible and palatable). Shina (stem) nalo huweza kutumika lakini labda sehemu changa kabisa kwa sababu ya changamoto ya tannins.
Majani haya hukaushwa juani ili kudhibiti madhara yatokanayo na asidi-amino ya mimosine ambayo ina athari kwa mifugo. Baada ya majani kupoteza kiasi cha maji ilichobeba, huwa tayari kwa ajili ya kuendelea na taratibu zingine za kuandaa chakula cha mifugo.
Majani ya Mlusina yaliyokaushwa
Chakula  kilichoadaliwa kwa ajili ya kuku huwekewa 5% ya majani ya mlusina, chakula kwa ajili ya nguruwe kinatakiwa kuwa na 10% tu ya mchanganyiko wa majani ya mlusina na chakula kinachoandaliwa kwa ajili ya ng’ombe kinatakiwa  kisichukue zaidi ya 30% ya mchanganyiko wa majani ya mlusina (Dongjing na Guodao, 1994).
Mlusina ni mzuri kwa sababu unapunguza gharama za kununua chakula cha kurutubishia mifugo(concentrates).


Hata hivyo, makala hii inajikita kwa matumizi ya Mlusina kwa ng'ombe. Maandalizi ya chakula kwa ajili ya ng'ombe yanatakiwa yasizidi 30%. Mfano kama chakula kinachoandaliwa ni kilo 100 maana yake ni kwamba majani ya Mlusina ambayo ni chanzo cha protini yanatakiwa yasizidi  kilo 30. Hata hivyo athari nyingi huonekana endapo asilimia za Mlusina zitazidishwa kwa kipindi kirefu, athari hizo ni kama vile kunyonyoka nywele(alopecia), matatizo katika ulaji(anorexia), kupoteza uzito, kutokwa na ute mdomoni(deep salivation), kuchubuka utumbo(esophagus lesions), kupoteza seli kwenye rumen na reticulum (necrotic papillae in the
rumen and reticulum), kuvimba kwa tezi (thyroid hyperplasia), kiasi kidogo cha homoni ya thyroxine(T4) kwenye damu, kifo cha kiinitete na vifo vya kabla na baada ya kuzaliwa (early embryonic mortality and perinatal death)  (Allison et al., 1992; Al-dehneh et al., 1994).

Ni vema mfugaji akawa na huu mmea ndani ya shamba lake kwa ajili ya mifugo yake kupata protini kwa wingi bila kutumia fedha nyingi kugharamia vyakula vya protini vinavyouzwa kwenye maduka mbalimbali ya vyakula vya mifugo.


No comments:

Post a Comment