Leo nimetamani kutoa maoni yangu juu ya migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji. Ni tatizo ambalo limekuwa sugu sana hapa nchini na pengine baadhi ya wananchi wakaamini hakuna suluhisho la hii migogoro. Kwanza, nikiri kwamba sikubaliani kwa namna yoyote na migogro hii kwa sababu imekuwa ikisababisha upotevu wa rasilimali kwa raia, jamii na serikali kwa ujumla, uharibifu wa mali, uhai wa raia na mifugo kwa ujumla. Lakini, hatuwezi kuacha kuongelea upotevu wa amani, ushirikiano kwenye jamii na kudumaza soko la mifugo na mazao yake hapa nchini na nje ya nchi.
Tukirejea katika mada, kwa miaka mingi katika nchi yetu tumekuwa tukiishi na jamii za kifugaji (pastoralists) kama wamasai na wasukuma. Wafugaji hawa wamekuwa wakitumia ufugaji wa asili nakuchangia katika ukuaji wa soko la nyama hapa nchini pamoja na kuchangia pato la taifa. Hata hivyo, japokuwa wamekuwa wakichangia pato la taifa kukua bado kuna takribani wafugaji milioni 10 wanaoishi katika umasikini (CGIAR, 2014).
Mahitaji makubwa ya mifugo ni malisho na maji na ndizo
zimekuwa sababu za ufugaji wa kuhama hama wafugaji kutoka eneo moja hadi
jingine wakitafuta mahitaji ya mifugo yao. Katika uhamaji wao ndipo
yanapotokea haya mapigano ya wafugaji na
wakulima. Hata hivyo katika jamii zetu lawama zote zimekuwa zikimrudia mfugaji
akionekana ndiyo chanzo cha migogoro hii. Serikali imezidi kujitahidi kumaliza
migogoro hii lakini imekuwa ikijirudia kwa sababu hakuna suluhisho la mahitaji
ya mfugaji katika eneo lake. Leo, ntafafanua baadhi ya mambo yanayochangia
migogoro hii tofauti na mfugaji kuwa chanzo cha moja kwa moja.
·
Kilimo
cha kuhama hama, tumekuwa tukishuhudia wakulima wengi wakilima bila kutumia
teknolojia ya kuhifadhi ubora wa udongo. Wamekuwa wakihama kufatana na ardhi
inavyopoteza ubora wa uzalishaji. Hii imechangia uharibifu wa ardhi, magugu
vamizi na upotevu wa maeneo ya machunga.
·
Watumiaji
wengine wa ardhi kuharibu mapalio ya mifugo, hizi ni njia za mifugo
zinazowafanya wafugaji kupitishia na mifugo kutoka eneo moja hadi lingine. Hata
hivyo maeneo haya yamekuwa yakivamiwa na wakulima katika upanuzi wa mashamba
yao na kusababisha migogoro wakati wa upitishaji wa mifugo kutokana na ufinyu
wa njia.
·
Dhana ya
eneo lenye chanzo cha maji ni zuri kwa kilimo cha umwagiliaji, ni kweli
kilimo cha umwagiliaji ni muhimu kwa ajili ya kuongeza uzalishaji. Lakini je,
vyanzo hivi vya maji vinatumika vipi kuhakikisha vinakidhi mahitaji kwa kuweka
miundo mbinu ya kuwezesha watumiaji wote kupata maji bila kuingiliana? Wakulima
wamekuwa wakilima na kuziba njia za mifugo kupitia kuelekea kwenye vyanzo vya
maji.
·
Uwekezaji
katika maeneo ya machunga, uwekezaji katika nchi yetu ni muhimu kwa ajili
ya maendeleo ya nchi yetu lakini kumekuwa hakuna mkakati maalum wa
kuwahakikishia wafugaji maeneo mbadala ya kuchungia mifugo. Hii hali huwafanya
kutanga tanga hovyo.
·
Upanuzi
na utambuzi wa maeneo ya hifadhi, tunatambua hakika rasilimali za nchi hii
ni muhimu sana kwa ajili ya kuongezea kipato taifa lakini pia kuhakikisha hata
vizazi vijavyo vinafaidika na rasilimali hizi za taifa. Lakini wafugaji
wamekuwa wakiondoshwa katika maeneo mbali mbali ili kuyafanya tengefu kwa
misitu au wanyama pori pasipo kuwatengenezea mbadala wa machunga. Baadhi ya
maeneo kama wildlife management areas (WMA) yamekuwa yakipandishwa hadhi na
kuwafanya wafugaji wakose machunga.
·
Ukosefu
wa elimu kwa wafugaji, elimu ya utunzaji na usimamizi wa machunga ni muhimu
kwa wafugaji ili waweze kuhudumia maeneo yao ya machunga.
·
Ukosefu
mpango mkakati wa kuboresha machunga na wataalamu wa malisho wa kutosha, hii
ni sababu ya wafugaji kuhama hama pia kwa sababu maeneo mengi yana vichaka,
magugu vamizi na vipara vingi. Mfugaji analazimika kuhama hama kutoka eneo moja
hadi jingine. Bahati mbaya hata mchakato wa kitaifa wa upigaji chapa hausaidii
kutatua changamoto za malisho bali utambuzi wa mifugo (identification). Maeneo tofauti
hapa nchini yana ikolojia tofauti. Mikakati maalum iwekwe ili kuboresha na
kulinda machunga kulingana na ikolojia zake.
·
Serikali
kutokutenga maeneo ya machunga kisheria, katika mipango bora ya ardhi,
serikali inatakiwa kutenga maeneo ya malisho na kuyatambua kisheria ili kuzuia
uvamizi unaofanywa na watumiaji wengine wa ardhi. Tunashuhudia maeneo ya misitu
na wanyama pori yakitengwa na kutambulika kisheria, hata maeneo ya machunga
yatengwe vivo hivyo.
Hizo ni baadhi tu ya sababu zinazo mfanya mfugaji kuhama
kutoka eneo moja hadi jingine. Ninaamini hakuna mfugaji anayependa kutembea
hovyo na mifugo, bali ukosefu wa malisho na maji unawalazimu kufanya ufugaji wa
kuhama hama kama maisha yao. Ukiangalia vizuri hizi sababu kidogo lawama kwa
wafugaji zitapungua. Kuna kila sababu ya kuangalia namna ya kutatua changamoto
zinazowasukuma wafugaji kuhama hama. Hapo tutapata suluhisho la migogoro hii.
14
No comments:
Post a Comment