Huu
ulikuwa ni mwaka ulioacha simanzi kubwa baina ya wafugaji ama jamii
zinazotegemea shughuli ya ufugaji kwa ajili ya kuendeshea maisha yao.
Simanzi hii imesababishwa na kuchelewa kwa mvua kulikosababisha
kukosekana kwa malisho na maji kwa kiasi kikubwa hapa nchini na
takribani ukanda wetu wote wa Afrika mashariki.
Ni ukweli usiopingika kwamba madhara yatokanayo na uchelewaji wa mvua za
vuli si mara ya kwanza kuyashuhudia hapa nchini. Kumekuwa na upotevu wa
idadi kubwa ya mifugo inayokufa sababu ya ukosefu wa malisho na maji
ndani ya msimu wa kiangazi. Lakini swali ni moja kwamba NI KWELI TUNAJIFUNZA KUTOKANA NA MAKOSA?.
Hapa hakuna wa kulaumiwa kuhusu mabadiliko ya tabia ya nchi lakini
alaumiwe yule mwenye uwezo wa kufikisha elimu ya kukabiliana na
mabadiliko ya tabia ya nchi. Katika nchi yetu kuanzia wasomi na hata
wale wasio na elimu ya darasani swala la kilimo cha malisho ni wimbo
usioeleweka masikioni mwao. Lakini je, tuache kuchukua njia sahihi kwa
sababu ya ukosefu wa uelewa juu ya swala hili?
Kilimo cha malisho ndio njia pekee ya kupambana na mabadiliko ya tabia
ya nchi. Ni njia itakayomwezesha na kumuhakikishia mfugaji uhakika wa
chakula cha mifugo wakati wa kiangazi. Mfugaji mwenye kuweza kudhubutu
kulima malisho atakuwa na uwezo wa kuvuna na kuweka akiba ya
malisho(kipindi cha msimu wa masika) na kutumia akiba hiyo kipindi cha
kiangazi wakati ambapo kuna upungufu mkubwa wa malisho. Jukumu hili
linabaki kwenye mamlaka husika kuhakikisha mbegu za malisho bora
zinapatikana ili elimu ya kilimo malisho iambatane na mbegu za malisho.
Katika kipindi hiki ambacho mifugo mingi inakufa tusiwalaumu wafugaji
kwa kuwaambia hawataki kuuza mifugo haswa msimu wa kiangazi wakati
tunajua mapungufu ya soko letu la mifugo na mazao yake. Tusiwalaumu
kutangatanga wakati tunajua hali ya machunga hapa nchini. Tunao uwezo wa
kukomboa ufugaji na ukaendelea kushamiri kwa wafugaji hawahawa
tunaowalaumu kila kukicha endapo tu mfumo mzima wa uendeshwaji na
usimamizi wa sera na sheria ukiwa sahihi. Tuhamasishe kilimo cha malisho
kwa wafugaji, tutumie mashamba darasa kuelimishia wafugaji hakika kilio
cha malisho msimu wa kiangazi tutakitokomeza.
No comments:
Post a Comment