By, Floidin John Linus, Emai. floidinjohn@gmail.com
Katika jamii yetu ya kitanzania mtu anaposikia neno UFUGAJI au WAFUGAJI
picha inayokuja kichwani kwanza ni NG'OMBE. Fikra ya kwanza haipeleki
mawazo kwenye mbuzi, kondoo, nguruwe, sungura, kuku au mifugo mingine.
Maana yake ni kwamba ufugaji katika jamii yetu unapeperushwa na nembo ya
NG'OMBE. Tunaposikia serikali ikitangaza ongezeko la mapato kutokana na
ufugaji, tunautizama mchango wa ng'ombe kwanza.
Lakini kujivuna kote kuhusu upatikanaji wa nyama, maziwa, ngozi na mazao
mengine ya mifugo yanategemea wafugaji hawa waliojaa sehemu mbalimbali
za nchi yetu katika mbuga wakichunga. Hata tunapotizama maduka ya nyama
katika miji mbalimbali ni mchango wa wafugaji hawa hawa wa asili.
Ufugaji sasa ni fursa kubwa sana kutokana na ongezeko kubwa la uhitaji
wa mifugo pamoja na mazao yake mbalimbali. Kwa bahati nzuri au mbaya
ufugaji wa nchini umeegemea zaidi kwa jamii kadhaa zilizo zoeleka tangu
awali kama jamii za kifugaji.
Kutokana na fursa hii wafugaji wamekuwa wakitumia ufugaji wao kwa ajili
ya kujipatia kipato chao kinachokidhi mahitaji yao ya kila siku.
Changamoto lukuki zinazokabili ufugaji hapa hatuwezi kuzipuuzia hata
kidogo katika kukwamisha maendeleo zaidi katika sekta hii ya mifugo.
Hivyo basi kutokana na uhitaji mkubwa wa mifugo na mazao yake kuna
namna mbili ambazo wafugaji wamekuwa wakitumia kuhakikisha wanafikia
uhitaji wa soko na kukidhi mahitaji yao.
1. Kuongeza idadi ya mifugo
2. Kuboresha mbinu za ufugaji.
1. KUONGEZA IDADI YA MIFUGO, hii ndiyo njia ambayo wafugaji wetu wa asili wamekuwa wakiitumia kuhakikisha kwamba wanafikia hitaji la soko pamoja na kulinda tamaduni (kijamii) zao.
Hata hivo haya mambo mawili yamekuwa na mchango mkubwa sana katika
kusababisha ongezeko la mifugo hapa nchini. Ongezeko hili linatokana na
changamoto za kibaiolojia na kimazingira
zinazo sababisha uzalishaji hafifu wa mifugo ya asili hivyo wafugaji
kuwalazimu kuongeza mifugo zaidi ili kupata mazao zaidi ya mifugo. Hata
hivyo ongezeko hili limekuwa na madhara makubwa katika mazingira
kutokana na uharibifu unaotokana na ardhi kushindwa kustahimili ongezeko
hili. Mmomonyoko wa ardhi, uharibifu wa nyanda za malisho, vyanzo vya
maji na huduma duni imekuwa ni changamoto kutokana na wingi wa mifugo.
Sababu kama vile,
- Mbegu duni za mifugo
- Ukosefu wa elimu ya kutosha kwa wafugaji wetu
- Mabadliko ya tabia ya nchi na
- Serikali kutotimiza majukumu yake ipasavyo, ni baadhi tu ya mambo yanayosababisha mfumo huu wa wafugaji kutumika kuongeza uwezo wa kupata zaidi mazao yamifugo.
2. KUBORESHA MBINU ZA UFUGAJI, huu kwa bahati mbaya siyo mfumo
tunaouona ukishamiri katika jamii tunazozitegemea kwa kiwango kikubwa
katika sekta ya ufugaji.Umekuwa ni
mfumo unaoshamiri zaidi kwa wajasiriamali wanaowekeza katika ufugaji.
Maana yake ni kwamba mfumo huu haujaweza kushawishi wafugaji wetu wa
asili. Yawezekana kabisa kwamba nguvu inayotumika kushauri wafugaji
haijakidhi mahitaji iongezewe nguvu ama haijaendana na uhitaji itafutwe
njia mbadala. Katika jambo hili, serikali nayo inachuku nafasi kubwa
sana kuzorotesha mfumo huu. Tukiangalia jitihada zilizofanyika wakati wa
awamu ya kwanza na baada ya azimio la Arusha tunaamini kama
zingeendelezwa basi leo hii tungeweza kuwa tunaongelea jamii za kifugaji
zenye ufugaji wa kisasa.
Huu ni mfumo ambao unaendana kabisa na mabadiliko ya dunia kwa sasa.
Unaendana na hitaji la soko kwa kuzalisha mifugo na mazao yake bora
kabisa kuweza kushindana katika masoko ya kimataifa. Lakini pia vilevile
ni mfumo rafiki kwa mazingira.
Mfumo huu unahitaji mabadiliko ya kifikra kwa wafugaji na nguvu ya
serikali na wadau wa mifugo kuhakikisha tunatoka katika ufugaji wa asili
na kuingia mfumo huu wa kisasa.
Ni mfumo wenye gharama sana lakini matunda yake ni makubwa zaidi kwa mfugaji,jamii na taifa kwa ujumla.
Swali la kujiuliza, ni nani atutegulie kitendawili hiki?. Jitihada
zipi zenye kuonekana na thabiti kutupa mwelekeo wa mabadiliko haya.
Kumlaumu mfugaji kutobadilika haisaidii bali kumwekea mfumo wa
kumwezesha ndiyo itasaidia, ,mfano, wataalamu wa kutosha, uwepo wa mbegu
bora za ng'ombe, madawa, soko na malisho bora (mbegu). KITENDAWILI HIKI
HAKINA MTEGUAJI KWA SASA. Hata serikali nayo inaingia kwa kusita sita,
vyama vya wafugaji ni hafifu na hata wadau wa sekta hii wamejiweka
pembeni na kutupia lawama kundi fulani.
Ufugaji ni fursa kubwa sana kama kuna nia ya dhati.
No comments:
Post a Comment