Sunday, 22 October 2017

MCHAKATO WA UPIGAJI CHAPA MIFUGO NI HITAJI LA SERIKALI, SIYO HITAJI MUHIMU LA MFUGAJI.

 Na, Floidin John Linus
 
Kwanza, ieleweke sipo tofauti na agizo la serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kuhusu upigaji chapa wa mifugo ili kufanya utambuzi wa mifugo nchi nzima. Yawezekana serikali inakerwa na migogoro ya kila mara kati ya wafugaji na wa kulima. Matatizo ambayo yamekuwa yakiligharimu taifa na jamii kwa ujumla. Na hatimaye kuzorotesha kasi ya mpango wa serikali kuendeleza sekta ya ufugaji hapa nchini.

Lakini mtizamo wangu ni kuhusu chimbuko la huu mchakato wa upigaji chapa kwa kila halmashauri. Kwa miaka mingi sekta ya mifugo hapa nchini imeshikiliwa na wafugaji wadogo wadogo wanaofuga kwa mfumo wa asili na kizamani. Hali hii imechangiwa na ufugaji kwa kufuata mifumo ya asili na kitamaduni. Hata hivyo, mfumo wa kuhama hama kutoka eneo moja hadi lingine kulingana na upatikanaji wa malisho na maji ndio umekuwa chanzo cha migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Hebu tutizame mfano, migogoro inayoendelea kati ya wafugaji na maeneo ya hifadhi za mapori tengefu na hifadhi za wanyama pori. Sheria zinazosimamia maeneo haya ziko wazi sana kueleza adhabu anazopewa yeyote anayedhubutu kuvunja taratibu za uhifadhi wa maeneo yale. Hata wafugaji tunaofikiri wana tatizo la ukosefu wa elimu wanatambua vizuri sana lakini jambo la kujiuliza ni kwanini wanaweka pembeni adhabu kali na kuhatarisha mifugo yao kwa kuziingiza maeneo yale yanayolindwa kisheria???? 

Kila mara taarifa zinasambaa za upigaji minada mifugo iliyokamatwa ndani ya mapori tengefu lakini bado wafugaji wanadhubutu kuingiza mifugo ili kupata malisho. Je ni kweli tatizo ni elimu? kiburi? au tatizo ni nini?. Sasa kwa taswira hii ya mfugaji kudhubutu kuingia kwenye maeneo yanayolindwa kisheria anashindwaje kuingiza kwenye shamba la mahindi ambalo mmiliki wake yuko nyumbani. Sijaribu kutetea uharibifu huu lakini kuelezea jinsi serikali inavyotumia mbinu ya upigaji chapa kudhibiti migogoro na mfumo wa ufugaji wa kuhama hama.
Wakati mchakato huu unaanza wafugaji wengi  walipinga suala hili na serikali ikaona jambo la kufanya ni kuwaelimisha. Yawezekana kutoa elimu ikaonekana imechochea mwitikio lakini yawezekana pia wafugaji kuwa na uoga wa maagizo na sheria ndiyo chanzo cha mwitikio unaoendelea kujitokeza.
Lakini ukitumia jicho la tatu kutafakari maisha baada ya upigaji chapa bado changamoto zinazomkabili mfugaji zitakuwa hazijatafutiwa ufumbuzi. Bali itabaki uvunjifu wa sheria kwa kuingiza mifugo katika mikoa mingine kutafuta malisho na kuadhibiwa kisheria.Siyo rahisi mfugaji mkoani Dodoma wakati wa ukame atizame mifugo yake ikifa kwa njaa wakati mkoani Morogoro kuna malisho ya kutosha. Simaanishi kwamba naunga mkono ufugaji wa kuhama hama lakini serikali inatibu ugonjwa kwa dawa isiyokuwa sahihi. 
Serikali kupitia wizara ya mifugo na uvuvi iangalie namna ya kutatua mahitaji ya wafugaji ambayo yako wazi ili kuepusha huu ufugaji wa kuhama hama. Mfumo wa sheria pekee hautasaidia kutatua changamoto zinazomkabili mfugaji aliye nyikani. Changamoto zao ni zilezile miaka yote, wanahama hama kutafuta malisho,maji na miundombinu lakini upigaji wa chapa hautatui kero zao kuu zinazowakabili na kusababisha uzalishaji hafifu kulingana na kiasi pamoja na kiwango kinachotakiwa cha mifugo na mazao yake.

Saturday, 14 October 2017

MIGOGORO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI, LAWAMA ASIBEBESHWE MFUGAJI PEKE YAKE.

Leo nimetamani kutoa maoni yangu juu ya migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji. Ni tatizo ambalo limekuwa sugu sana hapa nchini na pengine baadhi ya wananchi wakaamini hakuna suluhisho la hii migogoro.  Kwanza, nikiri kwamba sikubaliani kwa namna yoyote na migogro hii kwa sababu imekuwa ikisababisha upotevu wa rasilimali kwa raia, jamii na serikali kwa ujumla, uharibifu wa mali, uhai wa raia na mifugo kwa ujumla. Lakini, hatuwezi kuacha kuongelea upotevu wa amani, ushirikiano kwenye jamii na kudumaza soko la mifugo na mazao yake hapa nchini na nje ya nchi.

Tukirejea katika mada, kwa miaka mingi katika nchi yetu tumekuwa tukiishi na jamii za kifugaji (pastoralists) kama wamasai na wasukuma. Wafugaji hawa wamekuwa wakitumia ufugaji wa asili nakuchangia katika ukuaji wa soko la nyama hapa nchini pamoja na kuchangia pato la taifa. Hata hivyo, japokuwa wamekuwa wakichangia pato la taifa kukua bado kuna takribani wafugaji milioni 10 wanaoishi katika umasikini (CGIAR, 2014).

Mahitaji makubwa ya mifugo ni malisho na maji na ndizo zimekuwa sababu za ufugaji wa kuhama hama wafugaji kutoka eneo moja hadi jingine wakitafuta mahitaji ya mifugo yao. Katika uhamaji wao ndipo yanapotokea  haya mapigano ya wafugaji na wakulima. Hata hivyo katika jamii zetu lawama zote zimekuwa zikimrudia mfugaji akionekana ndiyo chanzo cha migogoro hii. Serikali imezidi kujitahidi kumaliza migogoro hii lakini imekuwa ikijirudia kwa sababu hakuna suluhisho la mahitaji ya mfugaji katika eneo lake. Leo, ntafafanua baadhi ya mambo yanayochangia migogoro hii tofauti na mfugaji kuwa chanzo cha moja kwa moja.
·         Kilimo cha kuhama hama, tumekuwa tukishuhudia wakulima wengi wakilima bila kutumia teknolojia ya kuhifadhi ubora wa udongo. Wamekuwa wakihama kufatana na ardhi inavyopoteza ubora wa uzalishaji. Hii imechangia uharibifu wa ardhi, magugu vamizi na upotevu wa maeneo ya machunga.
·         Watumiaji wengine wa ardhi kuharibu mapalio ya mifugo, hizi ni njia za mifugo zinazowafanya wafugaji kupitishia na mifugo kutoka eneo moja hadi lingine. Hata hivyo maeneo haya yamekuwa yakivamiwa na wakulima katika upanuzi wa mashamba yao na kusababisha migogoro wakati wa upitishaji wa mifugo kutokana na ufinyu wa njia.
·         Dhana ya eneo lenye chanzo cha maji ni zuri kwa kilimo cha umwagiliaji, ni kweli kilimo cha umwagiliaji ni muhimu kwa ajili ya kuongeza uzalishaji. Lakini je, vyanzo hivi vya maji vinatumika vipi kuhakikisha vinakidhi mahitaji kwa kuweka miundo mbinu ya kuwezesha watumiaji wote kupata maji bila kuingiliana? Wakulima wamekuwa wakilima na kuziba njia za mifugo kupitia kuelekea kwenye vyanzo vya maji.
·         Uwekezaji katika maeneo ya machunga, uwekezaji katika nchi yetu ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu lakini kumekuwa hakuna mkakati maalum wa kuwahakikishia wafugaji maeneo mbadala ya kuchungia mifugo. Hii hali huwafanya kutanga tanga hovyo.
·         Upanuzi na utambuzi wa maeneo ya hifadhi, tunatambua hakika rasilimali za nchi hii ni muhimu sana kwa ajili ya kuongezea kipato taifa lakini pia kuhakikisha hata vizazi vijavyo vinafaidika na rasilimali hizi za taifa. Lakini wafugaji wamekuwa wakiondoshwa katika maeneo mbali mbali ili kuyafanya tengefu kwa misitu au wanyama pori pasipo kuwatengenezea mbadala wa machunga. Baadhi ya maeneo kama wildlife management areas (WMA) yamekuwa yakipandishwa hadhi na kuwafanya wafugaji wakose machunga.
·         Ukosefu wa elimu kwa wafugaji, elimu ya utunzaji na usimamizi wa machunga ni muhimu kwa wafugaji ili waweze kuhudumia maeneo yao ya machunga.
·         Ukosefu mpango mkakati wa kuboresha machunga na wataalamu wa malisho wa kutosha, hii ni sababu ya wafugaji kuhama hama pia kwa sababu maeneo mengi yana vichaka, magugu vamizi na vipara vingi. Mfugaji analazimika kuhama hama kutoka eneo moja hadi jingine. Bahati mbaya hata mchakato wa kitaifa wa upigaji chapa hausaidii kutatua changamoto za malisho bali utambuzi wa mifugo (identification). Maeneo tofauti hapa nchini yana ikolojia tofauti. Mikakati maalum iwekwe ili kuboresha na kulinda machunga kulingana na ikolojia zake.
·         Serikali kutokutenga maeneo ya machunga kisheria, katika mipango bora ya ardhi, serikali inatakiwa kutenga maeneo ya malisho na kuyatambua kisheria ili kuzuia uvamizi unaofanywa na watumiaji wengine wa ardhi. Tunashuhudia maeneo ya misitu na wanyama pori yakitengwa na kutambulika kisheria, hata maeneo ya machunga yatengwe vivo hivyo.

Hizo ni baadhi tu ya sababu zinazo mfanya mfugaji kuhama kutoka eneo moja hadi jingine. Ninaamini hakuna mfugaji anayependa kutembea hovyo na mifugo, bali ukosefu wa malisho na maji unawalazimu kufanya ufugaji wa kuhama hama kama maisha yao. Ukiangalia vizuri hizi sababu kidogo lawama kwa wafugaji zitapungua. Kuna kila sababu ya kuangalia namna ya kutatua changamoto zinazowasukuma wafugaji kuhama hama. Hapo tutapata suluhisho la migogoro hii.


  • 14

Thursday, 12 October 2017

Udongo wenye rutuba ni chanzo cha malisho bora.

Unapohitaji kujikita katika ufugaji kwa mlengo wa kibiashara yaani kuzalisha mifugo au bidhaa za mifugo kitu muhimu cha kujiuliza ni chakula cha mifugo. 
Mfugaji anaweza fikiria chakula katika mfumo wa nyasi kavu (hay) au nyasi mbichi. Hata hivyo wafugaji wengine wanaweza kufikiri mbali na kuamua kulima nyasi zao binafsi kwa ajili ya mifugo au/na kuuza. 
Tofauti na wengi wanavyofikiri, mahitaji ya mbolea katika uzalishaji wa nyasi ni makubwa kama katika uzalishaji wa mazao ya kawaida. 
Udongo wenye rutuba ya kutosha na matumizi sahihi ya mbolea huweza kutoa kiasi kingi cha malisho ya mifugo.

Mfugaji kabla ya kulima shamba kwa ajili ya malisho anashauriwa kutafuta wataalamu wa malisho ili kuweza kumsaidia kufanya utafiti katika eneo husika. Hata hivyo kwa kujikita katika rutuba ya udongo na uzalishaji, aina tofauti za nyasi huitaji mazingira tofauti ya kiwango cha madini ndani ya udongo. Si vyema mkulima kuamua kulima nyasi bila kupata ushauri wa kitaalamu. 

Katika kilimo cha nyasi changamoto ya rutuba kwenye udongo kwa kiasi kikubwa ni Nitrojeni (N), ikifuatiwa na Fosiforasi(P), Potashiamu (K) na salfa(S) kwa nadra sana katika udongo wa kichanga.
Katika udongo wenye rutuba nzuri ukiambatana na kilimo cha umwagiliaji wa nyasi au mvua ya kutosha tunategemea kupata malisho mengi zaidi kwa sababu nyasi zitapata rutuba na maji ya kutosha. Hata hivyo, maeneo yenye kutegemea mvua tu kama ardhi ina rutuba ya kutosha bado uzalishaji wa nyasi unakuwa ni mzuri.
Virutubisho vyote ambavyo mwanadamu anategemea kutoka kwenye nyama vinatokana na virutubisho ambavyo vinachangiwa na malisho anayokula mnyama pia. Lazima mfugaji apate malisho bora ili kuzalisha mifugo na mazao yake yenye ubora wa juu pia.


Mfugaji unaweza kuona kwa namna gani rutuba ya udongo ni muhimu katika ufugaji. Katika nchi yetu si rahisi kupata wafugaji wataoweza kufanya kilimo cha malisho cha umwagiliaji bali wengi wanategemea mvua za msimu hivyo lazima kujikita katika ubora wa udongo na elimu ya utunzaji wa udongo ili kutoruhusu upotevu wa rutuba. 
Kwa hakika mfugaji akiweza kudhibiti upotevu wa ubora na rutuba ya udongo tunategemea kupata matokeo chanya kwa kutegemea tu mvua ya msimu. Ni rahisi kugundua upungufu wa madini katika udongo kwa kuangalia viashiria kadha wa kadha katika uoto wa juu ya ardhi lakini hii inahitaji utaalamu na uzoefu pia.
Hata hivyo, siyo kila uzalishaji hafifu katika malisho husababishwa na upungufu wa rutuba pekee katika udongo. Mkulima/mfugaji anatakiwa kupata ushauri wa kitaalamu kabla ya kuamua kutumia mbolea katika uboreshaji wa kilimo cha malisho.

Monday, 9 October 2017

TUJIFUNZE KULINGANA NA MAKOSA.

Huu ulikuwa ni mwaka ulioacha simanzi kubwa baina ya wafugaji ama jamii zinazotegemea shughuli ya ufugaji kwa ajili ya kuendeshea maisha yao. Simanzi hii imesababishwa na kuchelewa kwa mvua kulikosababisha kukosekana kwa malisho na maji kwa kiasi kikubwa hapa nchini na takribani ukanda wetu wote wa Afrika mashariki. Ni ukweli usiopingika kwamba madhara yatokanayo na uchelewaji wa mvua za vuli si mara ya kwanza kuyashuhudia hapa nchini. Kumekuwa na upotevu wa idadi kubwa ya mifugo inayokufa sababu ya ukosefu wa malisho na maji ndani ya msimu wa kiangazi. Lakini swali ni moja kwamba NI KWELI TUNAJIFUNZA KUTOKANA NA MAKOSA?. Hapa hakuna wa kulaumiwa kuhusu mabadiliko ya tabia ya nchi lakini alaumiwe yule mwenye uwezo wa kufikisha elimu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi. Katika nchi yetu kuanzia wasomi na hata wale wasio na elimu ya darasani swala la kilimo cha malisho ni wimbo usioeleweka masikioni mwao. Lakini je, tuache kuchukua njia sahihi kwa sababu ya ukosefu wa uelewa juu ya swala hili? Kilimo cha malisho ndio njia pekee ya kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi. Ni njia itakayomwezesha na kumuhakikishia mfugaji uhakika wa chakula cha mifugo wakati wa kiangazi. Mfugaji mwenye kuweza kudhubutu kulima malisho atakuwa na uwezo wa kuvuna na kuweka akiba ya malisho(kipindi cha msimu wa masika) na kutumia akiba hiyo kipindi cha kiangazi wakati ambapo kuna upungufu mkubwa wa malisho. Jukumu hili linabaki kwenye mamlaka husika kuhakikisha mbegu za malisho bora zinapatikana ili elimu ya kilimo malisho iambatane na mbegu za malisho. Katika kipindi hiki ambacho mifugo mingi inakufa tusiwalaumu wafugaji kwa kuwaambia hawataki kuuza mifugo haswa msimu wa kiangazi wakati tunajua mapungufu ya soko letu la mifugo na mazao yake. Tusiwalaumu kutangatanga wakati tunajua hali ya machunga hapa nchini. Tunao uwezo wa kukomboa ufugaji na ukaendelea kushamiri kwa wafugaji hawahawa tunaowalaumu kila kukicha endapo tu mfumo mzima wa uendeshwaji na usimamizi wa sera na sheria ukiwa sahihi. Tuhamasishe kilimo cha malisho kwa wafugaji, tutumie mashamba darasa kuelimishia wafugaji hakika kilio cha malisho msimu wa kiangazi tutakitokomeza.

HUKU NDIKO TUNAKOTAMANI WAFUGAJI WETU WAFIKE.

Na, FLOIDIN JOHN LINUS                                  floidinjohn@gmail.com

Ni ukweli usiopingika kwamba wafugaji wengi wa kitanzania ni wale wenye shughuli hii kama asili yao mfano wasukuma na wamasai. Jamii hizi ndizo zimekuwa chanzo kikubwa cha mifugo na mazao ya mifugo katika masoko na minada yetu hapa nchini na nje ya nchi. Lakini kama ufugaji ndio utamaduni wao je, ni kweli tuna sababu ya kupoteza utamaduni wao? Jibu ni hapana,bali kusaidia kuboresha mfumo wa ufugaji kuhakikisha kuwa mfugaji anafaidika na ufugaji wake wa kila siku kwa ajili ya kuongeza kipato na kustawisha uchumi wa nchi. Mambo makuu mawili kwa mfugaji wa kitanzania yanayomkuba ni mabadiliko ya tabia nchi pamoja na ongezko kubwa la watu ambalo linazidi kuimega ardhi ya malisho kwa shughuli mbalimbali kama makazi na kilimo. Kuendana na hali hii ya mabadiliko kuna kila sababu ya mfugaji kuona sasa umuhimu wa kujikita katika kilimo cha malisho ya mifugo. Hii ina maana kwamba mfugaji atatakiwa kununua ardhi na kujikita katika kilimo cha malisho ili kuhakikisha ustawi wa mifugo yake kwa mwaka mzima. Kilimo hiki kinahitaji ushauri wa kitaalamu haswa kuweza kutambua aina ya majani yanayoweza kustahimili kulingana na eneo analopatikana mfugaji. Ni kweli kuna gharama zake lakini faida yake ni kubwa zaidi kuliko kutangatanga na mifugo katika kipindi ambacho malisho hayapatikanai. .Kilimo cha malisho kinampa mfugaji uwezo wa kuvuna nyasi hadi mara nne kwa mwaka na kujitengenezea uwezo mkubwa wa kuhudumia mifugo yake. Aidha, kilimo cha malisho kitapunguza kutembeza mifugo umbali mrefu zaidi kwa ajili ya kutafuta malisho jambo ambalo huharibu ubora wa nyama, hudhoofisha mifugo na kuipunguzia uwezo wa kuzaliana (reproductive efficiency). Katika msimu wa mvua malisho huwa ni mengi sana, uwezo wa ardhi kuzalisha malisho huongezeka na hivyo mifugo hupata chakula kiurahisi, lakini huu ndio msimu ambao wafugaji wetu wanatakiwa kujifunza namna ya kuhifadhi chakula kwa ajili ya baaadae. Mfano kuacha baadhi ya maeneo bila kuyachunga hadi msimu wa kiangazi ndio yachungiwe ili kuilinda mifugo hadi msimu mwingine.
. Mfugaji anaweza kuvuna pia nyasi na kuziandaa kwa ajili ya hei(HAY) baadae kuzifunga vizuri na kuzitunza hadi msimu wa kiangazi ambapo hakuna malisho kwa wingi. Kama mfugaji atakuwa na uwezo wa kuvuna mara nne kwa mwaka, manake atakuwa na uwezo wa kuzalisha hay nyingi zaidi ili kuilinda mifugo yake msimu wa kiangazi isihangaike na chakula.
. Njia nyingine ni katika mfumo wa saileji(silage), inahitaji utaalamu zaidi lakini mfugaji akiweza kuelekezwa tu basi anaweza kuhifadhi chakula cha mifugo kwa mfumo huu pasipo kupoteza ubora wa chakula hicho. Huku ndiko tunakotamani tuwaone wafugaji wakiamkia huku na kunufaika na ufugaji. Mifugo ni utajiri lakini uelewa huu ni tafsiri iliyo mbali na wafugaji wetu. Dhana ya wingi wa idadi ya mifugo ndiyo dhamira ya wafugaji. Lakini kama wakiruhusu utaalamu uingilie katikati yao watavuna zaidi kwa idadi ndogo tu ya mifugo. Tunayo safari ndefu ya kufika tunakotamani cha msingi ni kutonyosheana mikono na kutafutiana chuki bali kuamka na kumsaidia mfugaji atoke huko aliko na twende naye karne ya 21 tunakokutizama katika mfumo wa kibiashara

MATUMIZI YA MOTO NDANI YA NYANDA ZA MALISHO.


Moto ni silaha mojawapo inayoweza kutumika kwa ajili ya kuboresha hali ya machunga kwa ajili ya mifugo iwapo tu utatumika kiusahihi na kwa kuzingatia taratibu za kutumia moto ndani ya machunga. Ijapokuwa matumizi ya moto ndani ya machunga yana madhara yake lakini zifuatazo ni faida za matumizi ya moto ndani ya machunga. 1.Kutumika kwa ajili ya kuondosha mabaki ya majani yaliyokauka au kujishikiza kwenye vichaka na miti. 2. Kudhibiti mimea vamizi haswa kwa kuua mbegu zinazozalishwa au zilizo kwenye udongo tayari kwa kuota. 3. Kuchochea ukuaji wa malisho haswa msimu wa vuli unapokaribia. 4. Kuvutia mifugo kuweza kula malisho katika sehemu ambazo haipendelei kwenda sababu ya malisho kukosa ubora na virutubisho. 5. Kuua na kudhibiti magonjwa na wadudu wasababishao magonjwa kwa mifugo. 6. Kutumika kuzuia moto usiotarajiwa(wildfire). 7. Kuboresha makazi kwa ajili ya wanyama wafugwao pamoja na wanyama pori n.k Aidha pamoja na hayo, kama ilivyoelezwa mwanzo, matumizi ya moto yana utaratibu wake ndani ya eneo la malisho ya mifugo ama wanyamapori. Lazima mtaalamu wa sayansi ya usimamizi wa nyanda za malisho ajiridhishe kwa kuangalia hali ya hewa, kiasi cha mvuke, aina ya eneo na aiana ya uoto nk. ndio aamue kuhusu kutumia moto kama silaha salama kurekebisha hali ya malisho.

NANI ATUSAIDIE ATEGUE KITENDAWILI HIKI?

By, Floidin John Linus,     Emai. floidinjohn@gmail.com

Katika jamii yetu ya kitanzania mtu anaposikia neno UFUGAJI au WAFUGAJI picha inayokuja kichwani kwanza ni NG'OMBE. Fikra ya kwanza haipeleki mawazo kwenye mbuzi, kondoo, nguruwe, sungura, kuku au mifugo mingine. 
Maana yake ni kwamba ufugaji katika jamii yetu unapeperushwa na nembo ya NG'OMBE. Tunaposikia serikali ikitangaza ongezeko la mapato kutokana na ufugaji, tunautizama mchango wa ng'ombe kwanza.
Lakini kujivuna kote kuhusu upatikanaji wa nyama, maziwa, ngozi na mazao mengine ya mifugo yanategemea wafugaji hawa waliojaa sehemu mbalimbali za nchi yetu katika mbuga wakichunga. Hata tunapotizama maduka ya nyama katika miji mbalimbali ni mchango wa wafugaji hawa hawa wa asili. 
Ufugaji sasa ni fursa kubwa sana kutokana na ongezeko kubwa la uhitaji wa mifugo pamoja na mazao yake mbalimbali. Kwa bahati nzuri au mbaya ufugaji wa nchini umeegemea zaidi kwa jamii kadhaa zilizo zoeleka tangu awali kama jamii za kifugaji.
Kutokana na fursa hii wafugaji wamekuwa wakitumia ufugaji wao kwa ajili ya kujipatia kipato chao kinachokidhi mahitaji yao ya kila siku. Changamoto lukuki zinazokabili ufugaji hapa hatuwezi kuzipuuzia hata kidogo katika kukwamisha maendeleo zaidi katika sekta hii ya mifugo.
Hivyo basi kutokana na uhitaji mkubwa  wa mifugo na mazao yake kuna namna mbili ambazo wafugaji wamekuwa wakitumia kuhakikisha wanafikia uhitaji wa soko na kukidhi mahitaji yao.
1. Kuongeza idadi ya mifugo   
2. Kuboresha mbinu za ufugaji.
1. KUONGEZA IDADI YA MIFUGO, hii ndiyo njia ambayo wafugaji wetu wa asili wamekuwa wakiitumia kuhakikisha kwamba wanafikia hitaji la soko pamoja na kulinda tamaduni (kijamii) zao.
Hata hivo haya mambo mawili yamekuwa na mchango mkubwa sana katika kusababisha ongezeko la mifugo hapa nchini. Ongezeko hili linatokana na changamoto za kibaiolojia na kimazingira zinazo sababisha uzalishaji hafifu wa mifugo ya asili hivyo wafugaji kuwalazimu kuongeza mifugo zaidi ili kupata mazao zaidi ya mifugo. Hata hivyo ongezeko hili limekuwa na madhara makubwa katika mazingira kutokana na uharibifu unaotokana na ardhi kushindwa kustahimili ongezeko hili. Mmomonyoko wa ardhi, uharibifu wa nyanda za malisho, vyanzo vya maji na huduma duni imekuwa ni changamoto kutokana na wingi wa mifugo. Sababu kama vile,
  • Mbegu duni za mifugo
  • Ukosefu wa elimu ya kutosha kwa wafugaji wetu
  • Mabadliko ya tabia ya nchi na
  • Serikali kutotimiza majukumu yake ipasavyo, ni baadhi tu ya mambo yanayosababisha mfumo huu wa wafugaji kutumika kuongeza uwezo wa kupata zaidi mazao yamifugo.
2. KUBORESHA MBINU ZA UFUGAJI, huu kwa bahati mbaya siyo mfumo tunaouona ukishamiri katika jamii tunazozitegemea kwa kiwango kikubwa katika sekta ya ufugaji.Umekuwa ni
mfumo unaoshamiri zaidi kwa wajasiriamali wanaowekeza katika ufugaji. Maana yake ni kwamba mfumo huu haujaweza kushawishi wafugaji wetu wa asili. Yawezekana kabisa kwamba nguvu inayotumika kushauri wafugaji haijakidhi mahitaji iongezewe nguvu ama haijaendana na uhitaji itafutwe njia mbadala. Katika jambo hili, serikali nayo inachuku nafasi kubwa sana kuzorotesha mfumo huu. Tukiangalia jitihada zilizofanyika wakati wa awamu ya kwanza na baada ya azimio la Arusha tunaamini kama zingeendelezwa basi leo hii tungeweza kuwa tunaongelea jamii za kifugaji zenye ufugaji wa kisasa. 
Huu ni mfumo ambao unaendana kabisa na mabadiliko ya dunia kwa sasa. Unaendana na hitaji la soko kwa kuzalisha mifugo na mazao yake bora kabisa kuweza kushindana katika masoko ya kimataifa. Lakini pia vilevile ni mfumo rafiki kwa mazingira. 
Mfumo huu unahitaji mabadiliko ya kifikra kwa wafugaji na nguvu ya serikali na wadau wa mifugo kuhakikisha tunatoka katika ufugaji wa asili na kuingia mfumo huu wa kisasa. 
Ni mfumo wenye gharama sana lakini matunda yake ni makubwa zaidi kwa mfugaji,jamii na taifa kwa ujumla.
Swali la kujiuliza, ni nani atutegulie kitendawili hiki?. Jitihada zipi zenye kuonekana na thabiti kutupa mwelekeo wa mabadiliko haya. Kumlaumu mfugaji kutobadilika haisaidii bali kumwekea mfumo wa kumwezesha ndiyo itasaidia, ,mfano, wataalamu wa kutosha, uwepo wa mbegu bora za ng'ombe, madawa, soko na malisho bora (mbegu). KITENDAWILI HIKI HAKINA MTEGUAJI KWA SASA. Hata serikali nayo inaingia kwa kusita sita, vyama vya wafugaji ni hafifu na hata wadau wa sekta hii wamejiweka pembeni na kutupia lawama kundi fulani. 
Ufugaji ni fursa kubwa sana kama kuna nia ya dhati.

TUJADILI KIDOGO KUHUSU NDOROBO (TSETSE FLY) TANZANIA

Ndorobo ni wadudu warukao ambao husambaza trypanosomes wasababishao magonjwa ya trypanosomiasis na nagana kwa mifugo na malale kwa binadamu. Kwa Tanzania trypanosomiasis ni kati ya magonjwa yanayoathiri binadamu na mifugo. Ndorobo wana madhara mengi sana kwa mifugo kama vile kuongezeka kwa vifo, mimba kutoka, kushuka kwa uwezo wa kuzaliana, ukuaji hafifu, uzalishaji hafifu wa nyama na maziwa, kuzuia matumizi ya machunga,kuongeza gharama za kuzuia ndorobo n.k. Kwa Afrika inakadiriwa kuwa ni kilomita za mraba milioni 10 zenye ndorobo ambapo kati ya hizo ni takribani kilomita za mraba milioni 7 zinazostahili kwa kulishia mifugo na eneo lililobaki likiwa ni misitu. Ni 40% ya eneo la Tazania lililoathiriwa na ndorobo ambalolingefaa kwa shughuli za kilimo na kuchungia mifugo. Aidha anasema ni takribani mifugo milioni 4.4 na watu milioni4 ambao wako kwenye nafasi kubwa ya kuambukizwa ugonjwa unaotokana na ndorobo. Inakadiriwa kuwa ni takribani US$ 7.98 milioni zinapotea kila mwaka kutokana na madhara yatokanayo na ndorobo (Malele,2011). Kwa kiasi hiki cha pesa inatoa nafasi kubwa kutafakari ni kwa jinsi gani taifa na wafugaji wanapoteza mapato kama tu ndorobo wangedhibitiwa. Tanzania inakadiriwa kuwa na spishi(species) kumi (10) za ndorobo ambazo zimetapakaa kulingana na uwezo wa kila spishi kustahimili eneo husika. Aidha inaelezwa kuwa, kubadilika kwa matumizi ya ardhi, ongezekola watu na shughulu zinazohusu binadamu ni kati ya vyanzo vya kusambaa kwa ndorobo hapa nchini. NJIA ZA KUDHIBITI NDOROBO
.
1. Kuondoa vichaka. Hii ni njia iliyoanza kutumika tangu enzi za ukoloni. Ilihusisha kuondoa aidha vichaka vyote au sehemu tu ya vichaka iliyoonesha kuwa kivutio ama makazi ya ndorobo. Kwa upande wa mazingira si rafiki sababu husababisha eneo kuwa wazi hivo kuwa na madhara mengi. Hivo haitumiki sana ijapokuwa inaweza kutumika kwa kuzingatia usalama wa mazingira. 2.2. Kutumia kemikali
Hii ni njia ya kutumia dawa ya kuulia wadudu ambapo inaweza kupuliziwa kutoka angani(aerial spraying) kwa kutumia vifaa maalumu ama kupuliziwa kutokea ardhini(ground spraying), kila njia ina madhara yake na faida zake na viumbe vingine pia huweza kuathirika kutokana na kemikali inayotumika kuua ndorobo.Kemikali zinazoweza kutumika ni Dieldrin (a residual organochloride), Endosulfan (Thiodan; a non-residual organochloride) na Synthetic pyrethroids. 3. Sterile male release technique
Hii ni njia inayotumika kwa kuandaa madume ya ndorobo ndani ya maabara.Madume haya huondolewa uwezo wa mbegu zake kutungisha halafu huachiliwa kwenye eneo liliothiriwa na ndorobo. Ni njia ya gharama sana. Ijapokuwa kutokana na (Bonomi et al., 2011),G. fuscipes ina onekana kuwa tofauti katika njia hii. Njia hufanya ufanisi zaidi kama eneo linalokusudiwa ni dogo pia idadi ya madume yaliyo ondolewa uwezo wa kutungisha maabara yanatakiwa kuwa na idadi kubwa kuliko madume yaliyoko eneo husika.
4. Kutumia mitego
Hutengenezwa kwa kutumia kitambaa cheusi na bluu. Rangi nyeusi huwavuta ndorobo na kutua kwenye rangi nyeusi hivyo kuweza kuvutwa kwenye kifaa cha kukusanyia au sehemu ilikopakwa kemikali ya kuua ndorobo. Lakini pia kemikali za kuwavutia kama acetone, mkojo wa ngombe au mbogo huweza kutumika sababu hutoa harufu ya kuwavuta. Kuzingatia, kuna mitego ya aina nyingi kulingana na aina(spishi) ya ndorobo.Hizo ni baadhi ya njia za kudhibiti ndorobo ambazo hutumika katika maeneo yaliyo athirika na ndorobo.

KUUZA MIFUGO ISIONEKANE KAMA TU NDIYO NJIA PEKEE YA KUKABIRI MSONGAMANO WA MIFUGO KWENYE MAENEO YA MACHUNGA.



Na, FLOIDIN JOHN LINUS                   floidinjohn@gmail.com

ARDHI ILIYOATHIRIWA NA SHUGHULI ZA UFUGAJI
Hapa lazima tuoneshe utofauti wa mtaalamu wa usimamizi na uendelezaji wa nyanda za malisho na wataalamu wengine.
Ni kweli ndani ya nchi yetu tunakabiriwa na maeneo yenye kuathiriwa na mikusanyiko ya mifugo eneo moja na kusababisha uharibifu wa mazingira na migogoro. Mikusanyiko hii chanzo chake ni katika hatua za utafutaji wa malisho, maji, kukimbia magonjwa ya mifugo na sababu zingine za kijamii. 
Mikusanyiko hii imeathiri ardhi na kusababisha mmomonyoko wa ardhi na makorongo, uharibifu wa vyanzo vya maji, migogoro ya mara kwa mara na uharibifu wa malisho.
Hata hivyo mikusanyiko hii imeonekana kuzidi kuongezeka kadri siku zinavyokwenda maana yake ni kwamba wafugaji wetu wanakumbana na changamoto nyingi machungani.
Ukisikiliza majadiliano ya watu wengi wanasema kuwa wafugaji wanatakiwa kutambua kuwa sasa ardhi imekuwa na matumizi mengi lazima wajifunze kutulia sehemu moja na kuzalisha kitaalamu na kisasa zaidi. Ni kweli lakini mabadiliko haya yanapofanyika wahusika wakuu hawaangalii mbadala wa wafugaji waliokuwa wanatumia maeneo haya, hatimaye hutoa nafasi ya wafugaji kutangatanga.
Mfugaji anakabiliwa na marekebisho ya matumizi ya ardhi yasiyojali mazingira rafiki ya shughuli yake. 
Ufugaji  unaonekana kama shughuli inayostahili kufanyiwa kwenye maeneo yasiyofaa kwa kilimo(remote & unproductive areas), lakini binafsi hii hoja huwa naipinga kwa sababu kuu mbili,
1)Tukisema ufugaji ufanyike katika maeneo yasiyofaa kwa kilimo, swali ni Je,katika karne hii yenye teknolojia za juu sana ni eneo gani lisilofaa kwa kilimo?. Mfano, teknolojia za umwagiliaji,mbegu bora za nafaka na mbolea.
2) Mahitaji ya malisho ni sawa kabisa na mazao ya nafaka, mfano mbolea ya kutosha na maji, vyote hivi hutimiza mahitaji ya mwili wa mnyama ili kufikia uzalishaji wenye tija zaidi na bora kwa mtumiaji.
Kwa kiwango kikubwa misongamano au mikusanyiko hii inasababishwa na watumiaji wengine wa ardhi wasiotoa mbadala wa mfugaji kupata mahitaji yake.
Mfano,
ü  Kumzuia mfugaji kuharibu vyanzo vya maji ni vizuri sana, lakini kumzuia mfugaji pasipo kumtengenezea njia mbadala ya kunyweshea mifugo yake pasipo kuathiri vyanzo vya maji ni mbaya zaidi.
ü  Kumwondosha mfugaji katika ardhi yenye rutuba ili kupanua shughuli za kilimo ni vema lakini kumwondosha bila kumwandalia sehemu nyingine yenye mahitaji stahiki ni kumwonea.
ü  Kumwondoa mfugaji ili apishe uwekezaji ni vema kwa uchumi wa nchi, lakini hatari ni pale asipoandaliwa eneo zuri la kuhamishiwa.
ü  Upanuzi wa maeneo tengefu(reserves) kwa ajili ya mapori na wanyama pori ni vizuri lakini unapomuondosha eneo husika unamtengenezea mbadala gani?
ü  Kukabidhi mamlaka ya vijiji kutenga maeneo ya malisho, ni vizuri lakini watu hawa wana elimu ya mifugo na wanajua ni maeneo gani na yenye sifa gani yanafaa kwa ajili ya mifugo?
Hiyo yote ni baadhi ya mifano inayosababisha mikusanyiko mikubwa ya mifugo kutokana na kukimbia sehemu mbalimbali zenye changamoto. Hivo ni ukweli kwamba kwa asilimia kubwa misongamano hii inasababishwa na watumiaji wengine wa ardhi japo mfugaji ndiye anaonekana tatizo.

            KUPUNGUZA  WINGI WA MIFUGO ENEO MOJA BILA KUUZA MIFUGO.
Hapa ndipo mtaalamu wa malisho anaweza kutofautiana na maamuzi ya wataalamu wasio wa machunga wasiojua sifa za mifugo kwenye machunga(grazing behavior).
Ø  Miundombinu ya maji, hii inaweza kuwa suluhisho la misongamano na kupunguza mikusanyiko ya mifugo kwenye machunga pasipo kuuza mifugo. Kupangilia umbali wa vituo vya maji(water sources) kulingana na aina ya mifugo iliyopo ndani ya machunga.Hii itasaidia kupunguza msongamano.
Ø  Kubadilisha maeneo ya kuchungia kufatana na umri, breed na spishi(species). Mfano, ndama wanaweza kuchungiwa maeneo yenye makorongo, mteremko mkali (rough terrain) hii pia itapunguza msongamano.
Ø  Kuwa na spishi tofauti ya mifugo hii itasaidia mifugo ya spishi tofauti kuweza kutumia aina tofauti ya aina ya mimea na maeneo tofauti.
Ø  Kagua eneo la machunga yawezekana msongamano wa malisho unasababishwa na uvamizi wa vichaka, mimea vamizi, magonjwa au wadudu hatarishi kama ndorobo n.k.

Utaalamu wowote ndani ya machunga ni vyema ukatizama kuongezea ardhi uwezo wa kuhudumia mifugo mingi zaidi ili kustawisha ufugaji hapa nchini.

KILIMO CHA MALISHO NI MUHIMU SANA KWA UFUGAJI WENYE TIJA

Gwatamala
Kitaalamu nyasi hizi huitwa  Tripsacum laxum.
Kwa kiingereza huitwa Guatemala grass.
Na kiswahili chake hujulikana kama   nyasi aina ya Gwatemala.
Asili yake ni kutoka nchini Mexico. Ni nyasi ambazo hudumu kwa muda mrefu(perennial), Huota na kukua kwa kusimama(erect) kwa urefu wa mita 2-3.
Huchomoza matawi kutoka kwenye vinundu(nodes) vya juu.
Hupandwa kwa kutumia vishina katika kipindi cha mwanzo wa msimu wa mvua.
Mfano wa vishina , kushoto ndiyo mfano wa kishina kilichoandaliwa kupandwa.

Hupandwa ndani ya mashimo ambayo yanakuwa umbali wa sentimita 50-65 kati ya shimo na shimo ili kutoa nafasi ya kutosha baina ya nyasi. Hupandwa katika mistari na kati ya mstari mmoja na mwingine iwe ni mita 100.
Mfano wa jinsi ya kupanda vishina  vya gwatamala.
Mfugaji anaweza kuandaa shamba na kupanda nyasi za gwatamala kwa ajili ya mifugo. Mahitaji ya kilimo hiki ni kwenye udongo wenye rutuba, Gwatamala huitaji  400 kg nitrogen, 80 kg phosphorus, 50 kg potassium, 50 kg calcium na 50 kg za magnesium kwa mwaka kwa hekta (Risopoulos, 1966).
Ijapokuwa nyasi hizi hupendelea sehemu zenye mvua ya kutosha lakini pia huweza kukua vizuri katika maeneo yenye udongo mzuri yanayopokea mvua kwa wastani wa 600mm kwa mwaka. Na wakati wa kiangazi hupunguza uwezo wa kuzalisha malisho. Hustahimili ardhi yenye asidi na aluminium lakini nyasi hizi hazistahimili maeneo yenye tatizo la kukumbwa na mafuriko.
Nyasi huweza kuwa tayari kuvunwa miezi sita baada ya kupandwa lakini huchukua tofauti ya miezi minne tu  kuvunwa msimu kwa msimu.
Ni nyasi nzuri kwa ajili ya ng'ombe wa maziwa kwa kukata na kulisha (green chop-chop for zero grazing) lakini pia nyasi za gwatamala zinaweza kutunzwa kwa mfumo sileji kwa ajili ya matumizi ya baadae katika msimu wa kiangazi.

MALISHO YENYE KUWEZA KUSTAHIMILI HALI YA UKAME.

NYASI ZENYE UWEZO WA KUSTAHIMILI MAENEO YENYE ASILI YA  UKAME

  1. Cenchrus ciliaris  (Buffel grass)
Buffel grass
Ni nyasi zinazolimwa sana kwa ajili ya kuzalisha
chakula cha mifugo. Zina uwezo wa kustahimili ukame kwa muda mrefu hivyo kupendekezwa kama nyasi zenye kuweza kulimwa maeneo kame hapa nchini kama Dodoma, Tabora na Singida. Hutoa mizizi yenye kwenda ardhini umbali wa hadi meta 2, hivyo huweza kufyonza maji ardhini mbali zaidi. Ni rahisi kupanda na hutoa malisho kwa wingi haswa zikipandwa na mbolea. Ikivunwa mwanzoni kabisa baada ya kuchomoza maua,huzalisha malisho mengi na bora ambayo huweza kutunzwa kama hei (hay). Akiba hii huweza kutumika wakati wa kiangazi kulishia mifugo. Buffel grass hustahimili moto (FAO, 2010). Haina uwezo wa kustahimili maeneo yenye kukumbwa na mafuriko (waterlogging area) na huweza kufa kwa baada ya takribani siku  6 (Ecoport, 2010). Huweza kuvumilia kuchungiwa (over grazing) hata kukanyagwa( trampling.

2. Urochloa mosambicensis
Sabi grass
Lugha za kawaida hujulikana kama Sabi grass (Australia), gonya grass (Zimbabwe) n.k.
Hizi ni nyasi zenye kustahimili ukame na kudumu zaidi ya mwaka mmoja (perennial). Hutofautiana kimo au wastani wa ukuaji pamoja na tabia (habit) ya ukuaji kutokana na sababu mbali mbali kama hali ya hewa ya eneo husika(climate), udongo (edaphic factors) n.k
Huota katika udongo tofauti ijapokuwa huitaji zaidi udongo wenye mbolea, kuanzia udongo wenye asili ya ufinyazi (clay soil) na ule wenye asili ya kichanga (sandy soil). Huweza kustahimili udongo  wenye asili ya u-asidi, alkali na chumvi chumvi.
Hata hivyo, kwa nchini mwetu wafugaji wetu hawajajikita katika ulimaji wa nyasi aina hii lakini ni chanzo kizuri cha chakula kwa ajili ya mifugo.
Ni nyasi ambayo haijathibitika kuwa na sumu yoyote kwa mifugo au kuwa na uhusiano na magonjwa, hivyo ni chakula kisicho na madhara kwa mifugo


3. Eragrostis superba (Masai love grass)
Masai love grass
Hujiotea kwa asili hapa nchini sababu ya wakulima au wafugaji wengi kutokujikita katika kilimo cha nyasi za kulishia mifugo.
 Hukua kwa haraka sana na huwa na hali ya umbijani kwa takribani mwaka mzima. Huweza kustahimili sehemu zenye udongo wa chumvi chumvi na alkali. Hustawi zaidi katika maeneo yenye udongo asili ya kichanga ijapokuwa hata udongo mwingine kama mfinyanzi hustawi. Hata hivyo ijapokuwa hukua haraka lakini hupoteza ubora(stemmy and unpalatable) kwa ajili ya mifugo kadri inavyozidi kukomaa pia kiwango cha virutubisho hushuka sana.
4. Bothriochloa insculpta ( Creeping bluegrass)
Creeping bluegrass
Hutumika kama nyasi za kuchungia au kutengenezea hei(hay)
 katika mashamba ya kufuga ng'ombe wa nyama (hukataliwa na ng'ombe wa maziwa).
Huweza kutumika kwa kuchungia au kukata nyasi na kulishia bandani (cut and carry). 
Ni bora zaidi kama hazijakomaa sana sababu ubora wake(palatability) hupungua kadri nyasi zinavyokomaa.
 Hustahimili ukame, kuchungiwa(heavy grazing) moto na 
mafuriko japo ni kwa kipindi kifupi tu. 
Huweza kustawi katika aina tofauti ya udongo japo haistawi vizuri maeneo yenye udongo wa kichanga . 
 Nyasi hizi hazistawi katika maeneo yenye kivuli au udongo wa asidi.
 MALISHO AINA YA MIKUNDE YENYE UWEZO WA KUSTAHIMILI MAENEO YENYE ASILI YA  UKAME
 1. Stylosanthes humilis

 Uwezo wake wa kutengeneza nitrojeni (nitrogen fixtion), kustahimili ukame, kuboresha hali ya udongo na kuwa chanzo cha protini kwa mifugo ni kati ya faida za huu mkunde. Mkunde huu una uwezo wa kutumia(extract) hata madini ya fosiforasi yaliyo  kidogo sana kutumika kwa ajili ya mimea mingine. Huweza kuoteshwa kwa kuchanganywa na baadhi ya nyasi zisizo zalisha kivuli kama vile Cenchrus ciliaris, Heteropogon contortus na Urochloa mosambicensis. Mkulima anaweza kuchungia moja kwa moja, kukata na kulishia bandani, kutengeneza hei au saileji. Hustahimili ukame pamoja na udongo wa kichanga au tifutifu. Hata hivyo, imethibitika mikunde hii kuwa sumu kwa baadhi ya kupe wasababishao magonjwa kwa ng'ombe (acaricidal effects) (Muro Castrejón et al., 2003; Fernandez-Ruvalcaba et al., 1999).
2. Stylosanthes hamata
Huu mkunde hauna utofauti na mkunde uliotangulia hapo juu katika ustahimilivu na matumizi yake kwa ajili ya mifugo.

Hayo ni baadhi ya malisho yawezayo kustahimili ukame na kuwa msaada kwa mfugaji.....

UMUHIMU WA MTI WA MLUSINA KATIKA UFUGAJI.

Leucaena leucocephala
Kwa jina la kisayansi unaitwa Leucaena leucocephala.
Kwa kiingereza huitwa Leucaena au Lead tree.
Kiswahili huitwa mti wa Mlusina.

Mmea huu jamii ya mikunde(leguminous) asili yake ni Mexico. Lakini hapa nchini pia hustawi vizuri kabisa. Ni kati ya miti yenye jamii ya mikunde inayokua kwa haraka sana. Ni chanzo cha chakula kwa mifugo . Hupandwa pembeni ya shamba kama kuonesha mpaka wa shamba, kutoa kivuli, kizuia upepo(wind breaker), kuzuia mmomonyoko wa ardhi au maalumu kwa ajili ya chakula cha mifugo. Mti huu ukiachwa kwa takriban mwaka 1.5 huruhusu mzizi mkuu kuingia ndani zaidi ya udongo hivyo  kuhakikisha uzalishaji wa chakulacha mifugo hata wakati wa kiangazi kipindi ambacho hakuna chakula cha kutosha au ubora wa malisho unapokuwa mbovu.
Shina laini na majani yake ni chanzo kizuri cha protini kwa mifugo na virutubisho vingine kama carotenoids na  vitaminslakini pia huambatana na asidi-amino iitwayo mimosine ambayo huwa  na athari endapo chakula kinachotokana na jamii hii ya mikunde kitatumiwa pasipo uangalifu, haswa wanyama wenye tumbo moja(monogastric) kama nguruwe, kuku na sungura huathirika zaidi na huweza kusababisha kifo kwa wanyama hawa.
Mlusina hufananishwa na mkunde mwingine (alfaalfa) muhimu kwa wingi wa virutubisho haswa protini kwa ajili ya mifugo. Lakini  Mlusina una upungufu wa sodium na iodine lakini una wingi wa b -carotene.

                                         MAANDALIZI YA MLUSINA KWA AJILI YA MIFUGO
Majani ya mlusina yaliyoandaliwa kama chakula cha mifugo
Maandalizi ya mlusina kwa ajili ya chakula cha mifugo huandaliwa kwa kuondoa majani pekee kutoka kwenye matawi ya mlusina. Ni kwa sababu ndiyo sehemu ya mmea huu yenye kuwa rahisi zaidi kutumiwa na mifugo(digestible and palatable). Shina (stem) nalo huweza kutumika lakini labda sehemu changa kabisa kwa sababu ya changamoto ya tannins.
Majani haya hukaushwa juani ili kudhibiti madhara yatokanayo na asidi-amino ya mimosine ambayo ina athari kwa mifugo. Baada ya majani kupoteza kiasi cha maji ilichobeba, huwa tayari kwa ajili ya kuendelea na taratibu zingine za kuandaa chakula cha mifugo.
Majani ya Mlusina yaliyokaushwa
Chakula  kilichoadaliwa kwa ajili ya kuku huwekewa 5% ya majani ya mlusina, chakula kwa ajili ya nguruwe kinatakiwa kuwa na 10% tu ya mchanganyiko wa majani ya mlusina na chakula kinachoandaliwa kwa ajili ya ng’ombe kinatakiwa  kisichukue zaidi ya 30% ya mchanganyiko wa majani ya mlusina (Dongjing na Guodao, 1994).
Mlusina ni mzuri kwa sababu unapunguza gharama za kununua chakula cha kurutubishia mifugo(concentrates).


Hata hivyo, makala hii inajikita kwa matumizi ya Mlusina kwa ng'ombe. Maandalizi ya chakula kwa ajili ya ng'ombe yanatakiwa yasizidi 30%. Mfano kama chakula kinachoandaliwa ni kilo 100 maana yake ni kwamba majani ya Mlusina ambayo ni chanzo cha protini yanatakiwa yasizidi  kilo 30. Hata hivyo athari nyingi huonekana endapo asilimia za Mlusina zitazidishwa kwa kipindi kirefu, athari hizo ni kama vile kunyonyoka nywele(alopecia), matatizo katika ulaji(anorexia), kupoteza uzito, kutokwa na ute mdomoni(deep salivation), kuchubuka utumbo(esophagus lesions), kupoteza seli kwenye rumen na reticulum (necrotic papillae in the
rumen and reticulum), kuvimba kwa tezi (thyroid hyperplasia), kiasi kidogo cha homoni ya thyroxine(T4) kwenye damu, kifo cha kiinitete na vifo vya kabla na baada ya kuzaliwa (early embryonic mortality and perinatal death)  (Allison et al., 1992; Al-dehneh et al., 1994).

Ni vema mfugaji akawa na huu mmea ndani ya shamba lake kwa ajili ya mifugo yake kupata protini kwa wingi bila kutumia fedha nyingi kugharamia vyakula vya protini vinavyouzwa kwenye maduka mbalimbali ya vyakula vya mifugo.